Taasisi zaonywa kumpuuza Wakili Mkuu

05Aug 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Taasisi zaonywa kumpuuza Wakili Mkuu

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba, amezitaka taasisi za umma zinazokataa kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zichukuliwe hatua kama zinafanya kosa la uhujumu uchumi.

Maagizo hayo aliyatoa jana jijini Dar es Salaam alipotembelea na kuzungumza na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata.

Awali, Wakili Malata alimlalamikia Dk. Mwigulu kwamba kuna baadhi ya taasisi za umma hazitoi ushirikiano wakati wa uandaaji wa hati za utetezi katika kesi mbalimbali zikiwamo zenye maslahi ya nchi, hivyo kusababisha wapate ushindi au kushinda kwa taabu.

"Inapotokea au itakapotokea taasisi zitakashindwa kutoa ushirikiano kwa makusudi na mara kwa mara, tuzijue na wachukuliwe kwamba, wanashiriki kuhujumu maslahi ya taifa,” alisema na kuongeza:

“Hii pia hata kwa mawakili wa serikali wanaotoa mwanya katika kuandaa kesi ili upande wa pili ushinde, lazima wafanyiwe assesment (tathmini) wasije kutuambia kwamba tumepigwa kitekiniko.”

Alisema vita ya kiuchumi hupiganiwa kisheria, kiakili, kimaandishi, hivyo yanapokuja maslahi ya nchi kuna upande mmoja tu kwao ambao ni ushindi.

"Vita ya kiuchumi haipiganiwi porini, hupiganiwa kwa kutumia akili na uwanja wa mapambano unakuwa sheria, mtu anabatilisha haki ya wengi kuwa ya yake binafsi, jukumu la kuingia katika vita ya kichumi ni sisi tuliokabidhiwa dhamana," alisema Dk. Mwigulu.

Aidha, aliitaka ofisi hiyo kuwa macho na kujipanga kuelekea kipindi cha uchaguzi kwa wale wanaotaka kupitisha mikono yao na watakaotaka kulipa fadhila za ‘mabwana zao’.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Amon Mpanju, alisema baada ya uchaguzi kunakuwa na mapingamizi mengi, hivyo alitaka ofisi hiyo ijipange.

Awali, Malata alisema ofisi yake imefanikiwa kuokoa Sh. trilioni 11.4 tangu ofisi hiyo kuanzishwa, na kwamba kama isingekuwapo zingeliwa kwa watu wasiostahili.

Habari Kubwa