Tabrofa waiomba Serikali machinjio ya kuku

23Oct 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Tabrofa waiomba Serikali machinjio ya kuku

CHAMA cha wafugaji wa kuku wa Nyama (Tabrofa), kimeiomba Serikali kujenga machinjio ya kuku na masoko maalum ya kuuzia kitoweo hicho kwa lengo la kuwaepusha na magonjwa.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Tabrofa, Coster Mrema, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya chama hicho yenye lengo la kuboresha ufugaji na uzalisha wa nyama bora nchini.

Amesema kutokana na kutokuwapo kwa masoko ya kuuzia, wanauza kuku hao kupitia kwa madalali ambao wanaenda kuchagua kwenye mabanda ambako wanawaachia magonjwa.

“Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imetenga maeneo maalum kuchinjia ng'ombe na mbuzi lakini hakuna machinjio ya kuku ni muhimu wajenge na kutenga maeneo katika masoko ili kuondokana na changamoto ya madalali kutulangua na kuleta magonjwa kwa kuku wakati wanapokuja kuchagua kwenye mabanda yetu," amesema Mrema.

Aidha, amesema Tabrofa kimepandisha bei ya kitoweo hicho, kutoka Sh. 5,500  hadi 6,000 kwa bei ya jumla na rejareja hadi Sh. 6,000 hadi 6,500 kwa bei ya jumla na rejereja.

Mrema amesema wamepandisha gharama za nyama ya kuku kwa sababu gharama za kutunza kifaranga hadi siku 28 zimepanda na kufika Sh. 5,600 ikiwamo chakula chanjo, umeme na maji.

“Lengo la kikao hiki ni kutangaza bei elekezi ya kuuza kuku ambao tutauza kwa Sh. 6,000 hadi 6,500 kuanzia sasa kutokana na gharama za chakula kuwa juu," amesema Mrema.

Mrema amesema pia wanaomba nyama za kuku ziuzwe kwa Kilogram badala ya kuuuza kuku mzima na gharama za vifaranga vishuke kutoka bei ya sasa ya 1,300 hadi iwe 1,000 ili kuwapunguzia mzigo wafugaji.

Amesema pamoja na mambo mengine chama hicho, kilianzishwa na kusajiliwa rasmi mwaka 2017 kwa lengo la kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji wa kisiasa bila kutumia dawa.

“Tunasema kufuga bila dawa inawezekana hivyo ni muhimu wafugaji wakatambua ufugaji wa kuzingatia usafi na mazingira salama ili kuzalisha vitoweo salama kwa afya ya Watanzania wote," amesema Mrema.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji wa Kuku wa  Mayai, alioomba Serikali kuruhusu soko la bidhaa hizo kuvuka mipaka ya Tanzania kwa lengo la kuinua uchumi wao na kukuza sekta ya uchumi nchini.

Habari Kubwa