TMA yatabiri mvua kubwa kuanzia leo

05Dec 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
TMA yatabiri mvua kubwa kuanzia leo

MVUA kubwa zinatarajia kunyesha ndani ya kipindi cha siku tano kuanzia leo kwenye mikoa 17 ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Samuel Mbuya

Kwa mujibu wa utabiri wa siku tano uliotolewa leo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua hizo zimeanza leo kwa baadhi ha maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na zitaendelea katika mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora, Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu na Shinyanga.

Meneja wa Huduma za Utabiri wa TMA, Samuel Mbuya, amesema kwa siku ya kesho mvua kubwa zinatarajiwa katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Iringa na Njombe.

"Athari zinazoweza kutokea ni kubwa hususani kwa baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kunaweza kutokea kwa uharibifu wa miundo mbinu, maeneo ha makazi kuzungukwa na maji na hali mbaya zaidi kwa wakazi wa maeneo ya mabondeni," alisema Mbuya.

Amesema hali ya maeneo ya makazi kuzungukwa na maji pia inatarajiwa kwa mikoa mingine iliyotajwa na hivyo shughuri za kiuchumi uwenda zikasimama.

Mbuya, amesema kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa zaidi kutokana na kuwepo kwa dalili ya vimbunga pacha katika bahari ya Hindi.

"Kuna mgandamizo mdogo wa hewa unaoendelea kuimarika vinavyotarajia kutengeneza vimbunga pacha magharibi mwa bahari ya Hindi na kuathiri mifumo ya hali ya hewa," amesema Mbuya.

Ameongeza kubwa vimbunga hivyo vinaonekana katika Pwani ya Somalia na Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Madagascar na kusababisha ongezeko la mvua kubwa katika Pwani ya kaskazini ya nchi yetu katika siku ya jana na leo.

Kutokana na matarajio hayo, TMA imetoa tahadhari kwa wananchi na Mamlaka husika juu ya athari zinazoweza kutokea na kuwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa wanazozitoa.

Habari Kubwa