Tahadhari mvua kubwa kunyesha

14Feb 2020
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Tahadhari mvua kubwa kunyesha

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa (juu ya wastani) baadhi ya mikoa ya Tanzania na Visiwani.

Mikoa hiyo imetajwa kuwa ni Dar es Salaam, Pwani, visiwa vya Pemba na Unguja na baadhi ya maeneo katika mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Mara huku mvua za wastani mpaka chini ya wastani (mvua ndogo) zikitarajiwa katika mikoa ya Kagera na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (Wilaya za Kakonko na Kibondo).

Kwa mujibu wa utabiri wa mvua za masika zilizotolewa jana na mamlaka hiyo kupitia kwa Mkurugenzi Dk. Agnes Kijazi, mvua hizo katika maeneo tajwa zinatarajia kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi na kuisha katika kipindi cha wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Mei.

Akizungumza wakati wa kutoa utabiri huo, Dk. Kijazi alisema mvua hizo kubwa zitasambaa mpaka katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

Dk. Kijazi, alisema mvua hizo hususani za juu ya wastani zinatarajiwa kuleta athari katika maeneo tofauti na kuzitaka mamlaka husika kuchukua tahadhari kukabiliana nazo.

“Yale maeneo ambayo yatapata mvua za wastani mpaka juu ya wastani tunategemea athari za kuharibika kwa miundombinu kutokea, pia usalama wa majisafi utaathirika kutokana na mvua zinazotarajiwa, hivyo Mamlaka za Miji zichukue tahadhari,” alisema Dk. Kijazi.

Alisema kwa upande wa sekta ya afya, wachukue tahadhari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko na malaria kwenye maeneo yatakayopata mvua za wastani mpaka juu ya wastani.

Aliitaka menejimenti ya maafa pia ichukue tahadhari kwa kuwa kuna uwezekano wa kutokea mafuriko kwa baadhi ya maeneo yatakayopata mvua kubwa na hivyo kusababisha upotevu wa maisha, uharibifu wa miundombinu na mali nyingine.

“Mamlaka inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, wasafirishaji na Mamlaka za Maji kuendelea kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika,” alisema Dk. Kijazi.

Alivita vyombo vya habari nchini kufuatilia mara kwa mara na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa na mirejeo pamoja na tahadhari na ushauri unaotolewa na TMA.

Habari Kubwa