Tahadhari ongezeko watoto wasiosikia

07Nov 2016
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Tahadhari ongezeko watoto wasiosikia

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imesema kuna ongezeko kubwa la watoto wenye matatizo ya usikivu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo matumizi yasiyo sahihi ya dawa ya malaria aina ya quinine.

Aidha, ongezeko hilo limechangiwa na magonjwa ambayo mama mjamzito huugua akiwa mjamzito, mtoto kuzaliwa na manjano au kupata ajali.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa huduma ya uwekaji programu ya usikivu kwa watoto 45, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Museru alisema tiba na vifaa hivyo huwa na gharama kubwa.

Alisema serikali kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ilitumia zaidi ya Sh. milioni 80 kwa mtoto mmoja kwa ajili ya kwenda nchini India kufanyiwa upasuaji kuweka kifaa cha usikivu.

Prof. Museru alisema hivi sasa huduma ya kuweka programu ya kifaa hicho inafanyika nchini baada ya wataalamu saba kurejea kutoka katika mafunzo ya siku 30 nje ya nchi.

"Lengo la serikali ni kupunguza gharama za matibabu nje ya nchi, na zitolewe hapa nchini," alisema Prof. Museru. "Kutokana na huduma hii sasa kutolewa MNH (serikali) imeokoa Sh. milioni 300 ambayo zingetumika kwa ajili matibabu haya."

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Ulisubisya Mpoki alisema wazazi wanatakiwa kutambua maendeleo ya ukuaji ya watoto wao ikiwamo afya.

Alisema idadi ya watoto wenye matatizo hayo wanaofikishwa katika hospitali hiyo ni ndogo ikilinganishwa na ambao wapo nyumbani au wazazi hawajawagundua.

Daktari Bingwa Wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo, Dk. Edwin Liyombo alisema tatizo hilo kwa watoto huweza kugundulika tangu umri wa miezi tisa baada ya kuzaliwa.

"Sababu za tatizo hili zingine hazijulikani, lakini dawa za quinine, gentamicine, ugonjwa atakaoupata mama akiwa mjamzito ni sababu nyingine, pia kuna baadhi wanazaliwa wakati 'air cells' zao hazipo vizuri ili kuruhusu usikivu," alisema.

Alisema watoto 45 wamekwishafanyiwa upasuaji wa kuweka programu ya usikivu, na kwamba ili kugundua watoto walio na tatizo hilo nchi nzima, Januari mwakani MNH itaanza kuwafanyia watoto uchunguzi tangu wanapozaliwa kwa kutumia vifaa maalumu.

Habari Kubwa