Tahadhari wanaume wenye VVU Kigoma

03Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Tahadhari wanaume wenye VVU Kigoma

WANAUME wanaoishi na mambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani hapa wapo hatarini kupoteza maisha yao kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ubishi wao uliopitiliza katika kuzingatia maelekezo ya kitaalamu ikiwamo kutumia kwa usahihi dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi (ARV).

Akifafanua jambo hilo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani juzi ambayo kwa mkoani hapa ilifanyikia

Ujiji, mwakilishi wa wanaume wanaoishi na VVU Manispaa ya Kigoma Ujiji, Athuman Rajabu, alisema wanaume wengi wenye VVU Kigoma wamebainika kuwa wako nyuma katika kuhudhuria vituo vinavyotoa huduma kwa ajili yao ni pia hukaidi kutwaa dawa na kuzitumia kwa usahihi.

“Ushiriki wa wanaume katika vituo vya huduma za tiba ni mdogo mno. Kuna baadhi huwatuma wenzi wao kuwachukulia dawa… lakini wanawake huwa hawajivungi kwenye umezaji wa vidonge, wapo wazi, si kama wanaume,” alisema Rajabu.

Rajabu alisema ili kupunguza tatizo hilo, jamii inapaswa kujiepusha na vitendo vya unyanyapaa dhidi ya watu waishio na VVU kwa sababu kinyume chake, baadhi ya waathirika watashindwa kujitangaza na hivyo kuendelea kuongezeka kwa mambukizi mapya nchini.

Mwakilishi wa wanawake wanaoishi na VVU, ambaye pia ni muelimishaji rika Kituo cha Afya cha Ujiji, Dafroza Francis,  aliikumbusha serikali ya wilaya ya Kigoma juu ya umuhimu wa kuimarisha huduma za msingi kwa watoto yatima  waishio na VVU.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma, Kwame Daftari, alisema serikali inatumia miongozo, mipango na sheria katika kutoa huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU na suala la huduma za elimu, lishe, mavazi na mengineyo husaidiwa kwa kiasi kikubwa na asasi za kiraia.

Awali, akisoma taarifa fupi  ya maambukizi ya VVU Manispaa ya kigoma Ujiji, Mratibu wa Idara ya Ukimwi, Laban Gwenyeza,  alisema yamepungua na kwamba sasa, watu 6,260 wenye VVU kati ya 13,215 wapo katika matumizi ya dawa.

Alisema kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2009/15, idadi ya walioambukizwa VVU walikuwa ni sawa na asilimia 4.8 lakini takwimu za sasa, ambazo ni za 2016/17, imebainika kuwa ni watu asilimia 1.9 tu wa Kigoma ndiyo waliobainika kuambukizwa VVU.