Taharuki Kariakoo ghorofa likiungua

14Jun 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Taharuki Kariakoo ghorofa likiungua

MOTO kwenye jengo la ghorofa moja lililopo katika makutano ya Mitaa ya Livingstone na Aggrey, eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ulizua taharuki kwa wapangaji, majirani na wapita njia jana.

Jengo hilo lenye fremu za maduka ya wafanyabiashara mbalimbali chini lilianza kuwaka moto majira ya asubuhi na kusababisha kiwewe kwa wafanyabiashara wenye mali, wakazi ghorofani, majirani na wapita njia.

Baada ya moto huo kuanza baadhi ya wenye maduka walionekana wakihangaika kuokoa mali zao huku wengine wakifunga maduka yao.

Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilifika eneo hilo muda mfupi baada ya moto huo kuanza na kufanikiwa kuudhibiti, ili usilete madhara zaidi kwa jengo zima na ya yale yaliyoko jirani.

Ingawa walifanikiwa kuuzima lakini picha mbalimbali zinaonyesha namna moto huo ulivyoteketeza jengo na baadhi ya mali zilizokuwamo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni,  alipoulizwa kuhusu chanzo na madhara, alisema taarifa kamili atazitoa baada ya uchunguzi na tathmini kufanyika.

"Ninachoweza kusema tukio limetokea, tumepata taarifa hiyo na tunafanya uchunguzi na tunafanya tathmini kujua hasara iliyopatikana," alisema Kamanda Hamduni. "Taarifa kamili tutaitoa tukikamilisha."

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkaguzi Joseph Mwasabeja, alisema changamoto waliyokutana nayo ni msongamano na namna ya kuingia kwenye eneo la tukio.

“Tahadhari tuliyotoa ni kwa wale waliokuwapo kwenye jengo husika, tumewaeleza wasiendelee na kazi hadi tumalize ukaguzi kama kuna usalama,” alisema.

Alisema maduka hayo yanajihusisha na vifaa vya plastiki hivyo walikuwa wanapambana na moto wa aina hiyo.

 

Habari Kubwa