Taharuki yazuka mtoto kuchomwa moto kwenye hifadhi Tabora

19Jun 2021
Halima Ikunji
Tabora
Nipashe
Taharuki yazuka mtoto kuchomwa moto kwenye hifadhi Tabora

Wananchi na wilaya Mkoani Tabora wamekumbwa na taharuki kubwa baada ya kuzagaa kwa taarifa za kuchomwa moto mtoto mdogo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya ISAWIMA iliyoko wilayani Kaliua Mkoani hapa.

Wananchi hao wakizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Mkoa huo wameeleza kusikitishwa na kitendo hicho kinachodhaniwa kufanywa na Maofisa Misitu wiki hii wakati wa oparesheni ya kuondoa wananchi waliovamia Hifadhi.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo Salome Luhingulanya alisema taarifa za tukio hilo zimewasikitisha sana kwani hata kama kuna watu wamevamia eneo hilo wangeweza kuondolewa kwa utaratibu unaoeleweka ikiwemo kupewa notisi.

‘Tulialikwa kwenye kikao na kupewa taarifa za tukio hilo ila hatukujua undani wake kwa kuwa Viongozi wa Chama tuliombwa tutoke nje ili kuipa nafasi Kamati ya Ulinzi na Usalama na Maofisa kutoka Wizara ya Maliasili kujadili suala hilo’, alisema.

Alisema kisheria hakuna mtu anayeruhusiwa kujenga makazi au kufanya shughuli zozote katika eneo la hifadhi, ila akabainisha kuwa kwa tukio la kuchomwa mtoto huyo anaamini mamlaka husika zitafanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika.

Mkazi wa Kaliua Yohana Lulandala alieleza kusikitishwa na taarifa za tukio hilo na kuomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini waliohusika kuchoma nyumba hizo na kupoteza maisha ya mtoto huyo aliyekuwa ndani na hatua za kisheria zichukuliwe pasipo kumwonea aibu mtu yeyote.

Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kutolea ufafanuzi suala hilo Kaimu Mkuu wa Mkoa huo Dkt.Philemon Sengati alikiri kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha wakati wa oparesheni ya kuondoa wavamizi wa hifadhi ya ISAWIMA.

Alisema kuwa hadi sasa haijathibitishwa ni nani aliyehusika kumchoma mtoto huyo kutokana na utata uliopo katika eneo hilo ila uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa ili kuabini wahusika ni akina nani huku akiahidi kutoa taarifa kamili.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa ACP Safia Jongo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa uchunguzi wa tukio unaendelea na utakapokamilika watatoa taarifa.