TAKUKURU Arusha imeokoa bilioni 1.36

25Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe Jumapili
TAKUKURU Arusha imeokoa bilioni 1.36

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, inatarajia kurejesha zaidi ya shilingi bilioni 1.36 ambazo zilikuwa ni fedha za umma na kodi mbalimbali za serikali zilizokuwa zimechukuliwa kwa njia ya rushwa kinyume na sheria.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, amesema kutoka katika fedha hizo atakabidhi zaidi ya shilingi  milioni 212 za mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma (PSSF).

Amesema shilingi milioni 293 zitakazotolewa zimetokana na uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo ambapo imeziokoa kutoka katika vitendo vya rushwa vilivyopelekea uingiaji wa mikataba mibovu pamoja na udanganyifu wa dhamana.

“Fedha hizi za umma za watumishi zilichepushwa kwa njia za rushwa na waajiri mbalimbali wasio waaminifu na hivyo kutaka kujinufaisha wao binafsi kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa”

"Fedha hizi pia ni sehemu ya shilingi bilioni 1.86 zilizotolewa kinyume na sharia na taratibu zinazosimamia vyama vya ushirika ikiwemo SACCOS ambapo SACCOS za Auwasa na AICC JIJINI Arusha zilipokea fedha hizo na kushindwa kurejesha fedha hizo serikalini kwa wakati” amesema Jenerali Mbungo.

Aidha, Jenerali Mbungo, amesema taasisi hiyo imefanikisha ulipwaji wa zaidi ya shilingi milioni 7.6 ambazo ni fedha za mfuko wa Taifa ya hifadhi ya jamii (NSSF) zilizotajwa kuwa ni makato ya watumishi yaliyopaswa kuwasilishwa NSSF katika tawi la Arusha kama ambavyo sharia inaelekeza lakini zilishukuliwa kwa njia ya rushwa na waajiri.

Habari Kubwa