TAKUKURU yaokoa Milioni 46 za walimu wastaafu

21Oct 2020
Dotto Lameck
Singida
Nipashe
TAKUKURU yaokoa Milioni 46 za walimu wastaafu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, imeokoa zaidi ya Shilingi Milioni 46 za pensheni ya walimu waliokuwa wamedhulumiwa na mkopeshaji haramu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi (kushoto) akimkabidhi Sh. 24,000,000/= Mwalimu Seleman Tyea Mwangu.

Walimu waliodhulumiwa ni Loth Mwangu ambaye alikuwa akifundisha katika shule ya msingi Ilonga na Selemani Tyea alikuwa mwalimu wa shule ya msingi Endasiku zilizopo wilayani Mkalama mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi (kushoto) akimkabidhi Sh.22,500,000/= Mwalimu Loth Mwangu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo kwenye ufunguzi wa mafunzo ya kupinga rushwa ya ngono kwa wananfunzi wa vyuo vikuu vya elimu ya juu, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, amesema walipokea malalamiko kutoka kwa walimu hao wastaafu ya kudhulumiwa fedha zao za pensheni na mkopeshaji aliyejulikana kwa jina moja la Bhoke kupitia mikopo umiza.

Mkuu wa TAKUKURU, Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda (wa pili kulia) akizungumza kabla ya walimu hao hawajakabidhiwa fedha zao.

Elinipenda amesema baada ya walimu hao kustaafu kwa nyakati tofauti walianza kukopa fedha kidogokidogo kutoka kwa mkopeshaji huyo na kufikisha jumla ya Shilingi Milioni 9 kwa mwalimu Loth na Milioni 2 kwa mwalimu Selemani, kwa makubaliano ya kulipa kupitia fedha za pensheni watakazolipwa. 

Baada ya mwalimu hao kupokea pensheni, mkopeshaji huyo waliwaongezea kiasi kikubwa cha riba tofauti na walivyokubaliana. Mwalimu Loth alidaiwa kulipa shilingi Milioni 22,500,00 kutokana na mkopo ambayo ni sawa na riba ya asilimia 215 huku Mwalimu Selemani akidaiwa kulipa Milioni 24 ambayo ni sawa na asilimia 1200, Nao wakalipa kupitia Benki ya NMB Tawi la Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akihutubia Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Mkoani humo.

Akizungumza baada ya kuwakabidhi fedha hizo walimu hao, Mkuu wa Mkoa huo wa Singida, Dk Rehema Nchimbi, amewataka wakopeshaji haramu mkoani humo kujisalimisha na wasipofanya hivyo mkono wa TAKUKURU na Dola utawakuta na hawatasalimika.

Habari Kubwa