TAKUKURU yaonya watumishi wa umma kujipitisha majimboni

09Apr 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
TAKUKURU yaonya watumishi wa umma kujipitisha majimboni

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewataka watumishi wa umma wanaopita katika majimbo ya uchaguzi kuanza sarakasi za uchaguzi kuacha vitendo hivyo mara moja kwa atakayebainika atachukuliwa hatua ikiwemo za kisheria.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Brigedia John Mbungo.

Aidha TAKUKURU imewaonya wanasiasa na wananchi kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ili kuhakikisha haki inatendeka katika Uchaguzi huo.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 9,2020 na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Brigedia John Mbungo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari pamoja na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Brigedia Mbungo amesema tayari kuna viashiria vya vitendo vya rushwa katika baadhi ya majimbo nchini ambayo taarifa zake zimeifikia taasisi hiyo na kuwaomba wananchi kujiepusha na rushwa hizo kutoka kwa wagombea na kutoa taarifa kwa taasisi hiyo wanapoona viashiria hivyo.

"Yapo mambo ya sintofahamu ambayo tayari yameanza kujitokeza majimboni na taarifa zake kubainishwa na Takukuru" amesema Brigedia Mbungo.

"Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inakemea harakati zote zinazofanyika mapema kabla ya kipenga cha kuanza kampeni kupulizwa " amesema

Mkurugenzi huyo pia ameonya watumishi wa Serikali kuingia katika shughuli za kisiasa kwa lengo la kutaka kuchaguliwa wakati ambapo bado ni mtumishi wa Serikali kwa kuwa kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa Sheria na kuwa kama mtumishi anataka kuingia katika siasa basi ni vyema akaachana na utumishi wa Serikali kwanza.

Kuhusu matumizi ya mfuko wa jimbo Mkurugenzi huyo amesema upo utaratibu ulioanishwa kwa mujibu wa Sheria ya Kusimamia Mfuko wa Kuhamasisha Maendeleo ya Jimbo ya mwaka 2009 na si kutumia vinginevyo huku akionya pia matumizi ya fedha binafsi za wabunge ili wasiingie katika mtego wa rushwa kwa kuwa ipo Sheria ya Kudhibiti Gharama za fedha za Uchaguzi ya mwaka 2010 itakayosimamia suala hilo.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2018/19 taasisi hiyo ilifanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 82.8 ambalo ni ongezeko la asilimia 6.7 kutoka kiasi cha shilingi bilioni 70.3 kwa mwaka wa fedha 2018/2019 huku miradi ya Maendeleo iliyofanyiwa ufuatiliaji nayo ikiongezeka kutoka miradi 691 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,494 hadi miradi 1,106 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,668.

Habari Kubwa