Takukuru kuja kivingine teknolojia uchaguzi mkuu

09Jan 2020
Julieth Mkireri
Kibaha
Nipashe
Takukuru kuja kivingine teknolojia uchaguzi mkuu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Pwani, imesema vifaa vitakavyotumika mwaka huu kuwakamata wanaotoa na kupokea rushwa ni vya kisayansi, na havionekani kwa macho.

Hayo yameelezwa jana, Mjini Kibaha na Mkuu wa Kitengo cha Elimu kutoka Takukuru, Frendick Mbigili, wakati akitoa mada kwenye semina ya wenyeviti wa serikali za mitaa Kibaha Mjini iliyoandaliwa na Tanzania Development Forum (TADEFO).

Mbigili alisema, vifaa vitakavyotumika mwaka huu wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu kubaini rushwa ni vya kisayansi, hivyo hakuna mtu anayeweza kuona kwa macho.

"Nyie wenyeviti ambao mpo madarakani kwa sasa tumeshirikiana sana wakati wa mchakato wa uchaguzi wenu, tunaamini tuko pamoja na nyie tunachowaomba ni kuendelea kuikataa rushwa katika majukumu yenu,” alieleza na kuongeza:

“Vyombo vya kisayansi vitatumika kubaini rushwa kwa mwaka huu, havionekani kwa macho na hutamjua nani anacho kwenye kundi lenu, kinachotumika ni kuikataa rushwa na kutekeleza majukumu yenu kwa uadilifu.”

Awali mmoja wa waalikwa katika semina hiyo Mchungaji Pascal Mnemwa, aliwatahadharisha wenyeviti kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa, kwani yamekuwa kero kwa jamii na kudumaza maendeleo.

"Hakuna imani inayosema rushwa inakubalika, viongozi wasiotimiza majukumu yao mara kwa mara wamekuwa wakitumia rushwa ili wananchi wawachague kwa kuwa hawana sifa za kuwa viongozi," alisema.

Mnemwa alisema ni vema wenyeviti wa mitaa wakasimamia kikamilifu kwenye jamii yao na kuacha kutumiwa na wagombea ambao hawana sifa za kukubalika kuongoza na badala yake wamekuwa wakilazimisha kutoa rushwa ili wapate nafasi wanazotaka.

Naye Shekhe Hamis Mtupa alitoa wito kwa viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa hofu ya Mungu.

Wenyeviti hao walimpongeza Tadefo kwa semina hiyo ambayo imewakutanisha na kubadilishana uzoefu katika majukumu yao.

Habari Kubwa