Takukuru yamsafisha Lusinde tuhuma za rushwa

15Jul 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Takukuru yamsafisha Lusinde tuhuma za rushwa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imemsafisha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtera Livingstone Lusinde baada ya kukosa uthibitisho kuhusiana na tuhuma za rushwa walizokuwa wanamtuhumu.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo.

Hivi karibuni, Taasisi hiyo ilitoa taarifa ya kumkamata Lusinde kwa tuhuma za kutoa rushwa ya fedha kwa wajumbe 20 ili kusaidiwa kwenye mchakato wa uchaguzi. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo amesema baada ya kufanya uchunguzi wao hawakufanikiwa kupata vithibitisho vilivyoonyesha kuwa walitoa rushwa.

Akizungumza mara baada ya kauli hiyo ya Takukuru, Lusinde amesema tuhuma hizo zilimsikitisha sana na anamshukuru Mungu kwa ukweli kuwekwa wazi.

“Nashukuru Mungu kwa taarifa iliyotolewa na Takukuru, nilikaa kimya kwa makusudi mimi nimekuwa kiongozi kwa miaka 10 nimekuwa Mbunge na Mjumbe wa NEC, unapopata tuhuma unatulia unaacha vyombo vya dola vifanye kazi yake,”amesema.

Amesema alikaa kimya kutoa nafasi kwa vyombo hivyo kufanya kazi yake ambapo wamejiridhisha na kubaini hakuna madai ya kutoa rushwa.

“Naendelea kuwaambia viongozi wanokutwa na kadhia hiyo wajitulize waache kujibishana na vyombo vya dola, naitaka Takukuru iendelee kuchapa kazi kama kawaida, wameendelee kufuatilia kila wanapopata taarifa, wanasiasa nasi tufanye kazi zetu kwa weledi na uwazi, taarifa imekuja wakati muafaka na kesho(leo) narudisha fomu,”amesema.

Hata hivyo amewataka watoa taarifa kuhakikisha wanatoa taarifa ambazo wanauhakika nazo ili kurahisisha uchunguzi.

Habari Kubwa