TAKUKURU yaokoa milioni 48/- za miradi

03Oct 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe Jumapili
TAKUKURU yaokoa milioni 48/- za miradi

​​​​​​​TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma imesema imeokoa fedha na vifaa vyenye thamani ya jumla ya Sh. milioni 47.8, vikiwamo vya Sh. milioni 41,8 vilivyochepushwa kutoka kwenye mradi wa ujenzi wa hospitali.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, alisema juzi jijini hapa kuwa hatua hiyo imetokana na ukaguzi wa miradi 17 ya sekta za elimu, afya na kilimo  uliolenga kuhakikisha fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi mbalimbali, zinatumika kwa ufanisi na uaminifu.

Alisema katika kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana, taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inaendelea kuelekeza nguvu katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara na maji kwa kuzuia vitendo vya rushwa na kufanya utambuzi wa mianya ya rushwa unaolenga kutoa ushauri wa namna ya kuziba mianya hiyo.

Kibwengo alibainisha kuwa Agosti mwaka huu, TARURA Mkoa wa Dodoma ilitia saini mikataba 43 na makandarasi mbalimbali kwa kazi ya ujenzi wa barabara katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma zenye thamani ya jumla ya Sh. bilioni 10.2 ikiwa ni miradi ya awamu ya kwanza itakayotekelezwa kwa mwaka 2021/22.

“RUWASA iligawanya mabomba yenye urefu wa mita 35,232 katika wilaya zote za Dodoma kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa mpango wa malipo kwa matokeo awamu ya nne ambapo gharama za ulazaji wa mabomba hayo zinakadiriwa kuwa zaidi ya Sh. milioni 95," alisema.

Sambamba na hayo, alisema katika kipindi cha robo iliyoisha, jumla ya taarifa 120 zimepokewa na taasisi hiyo ambapo taarifa za rushwa zilikuwa 76 huku taarifa sita kati ya hizo zikihamishiwa idara nyingine.

“Uchunguzi wa majalada 10 ulikamilika na mashauri tisa yakafunguliwa mahakamani ambapo mashauri sita yalitolewa hukumu na Jamhuri imeshinda mashauri matatu na kushindwa matatu," alifafanua.

Kibwengo alisema kuwa katika robo mwaka inayofuata, yaani Oktoba hadi Desemba mwaka huu, TAKUKURU itatumia mbinu ya kuwashirikishwa vijana katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia ushirika wa UTATU WA TAKUKURU.

Alikumbusha kuwa utatu huo unajumuisha Chama cha Skauti Tanzania pamoja na Idara ya Elimu kwa kuwaelimisha kuhusu mbinu na umuhimu wa kushiriki katika kuzuia rushwa ili nao wafikishe elimu nyumbani na jamii kwa ujumla wake.

"Kazi yetu ni kuhakikisha jamii inakuwa salama dhidi ya vitendo vya rushwa, tunaendeleza mapambano kupitia programu yetu ya TAKUKURU INAYOTEMBEA kwa kufuata wananchi na kusikiliza kero zao zinazohusiana na rushwa na kuzitafutia ufumbuzi. Vilevile, tutaendelea na jukumu la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa wetu," alisema.

Habari Kubwa