Takukuru yapokea malalamiko 169

30Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Takukuru yapokea malalamiko 169

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Morogoro imesema imepokea jumla ya taarifa za malalamiko 169 ya sekta mbalimbali kutoka kwa wananchi huku sekta ya ardhi ikiongoza kwa kuwa na malalamiko 32 kati ya sekta 20 zilizolalamikiwa.

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Morogoro Manyama Tungaraza alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mwaka 2021 mbele ya waandishi wa habari kuwa kati ya taarifa hizo 169, taarifa 67 zinahusiana na makosa ya rushwa na uchunguzi wake uko katika hatua mbalimbali  na kwamba taarifa 102 hazikuhusiana na makosa ya rushwa na hivyo walalamikaji kupewa ushauri wa namna ya kutatua kero zao.

Alisema sekta ya ardhi imeongoza kwa kuwa na malalamiko 32 ikifuatiwa na sekta ya TAMISEMI – Utawala na kwamba sekta ya Usafirishaji na sekta ya Maliasili zimefungana kwa kupata malalamiko 2 kila moja na kushika nafasi ya mwisho.  

Tungaraza alisema sekta ya Ardhi imeshika nafasi ya kwanza kulalamikiwa katika masuala mbalimbali ikiwemo ucheleweshwaji wa kesi kwenye mahakama za ardhi, urasimishaji wa ardhi na uvamizi wa ardhi.

Wakati huo huo Tungaraza alisema TAKUKURU imefanikiwa kushinda kesi 9 na kushindwa kesi moja kati ya kesi 10 za Jamhuri zilizohukumiwa mkoani Morogoro.

Alisema pia Taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 17 waliofunguliwa kesi 17 katika mahakama mbalimbali zilizopo mkoani hapa zikiwemo kesi 3 kwenye mahakama ya mkoani Morogoro, wilayani Gairo kesi 6, Kilombero kesi 4, Ulanga kesi 3 na Malinyi kesi 1.

Tungaraza alisema mpaka sasa kesi 47 zinaendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali zilizopo mkoani Morogoro.

Habari Kubwa