Takukuru yatahadharisha wanaotegemea mikato, upendeleo

10Dec 2016
Anceth Nyahore
KAHAMA
Nipashe
Takukuru yatahadharisha wanaotegemea mikato, upendeleo

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa maalum wa Kahama, imewataka wananchi kubadili tabia na kuacha kupata huduma kupitia njia za mkato na upendeleo.

Aidha imewaonya kuachana na woga ili kupata huduma stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi na wasitegemee kuhudumiwa kwa kutoa kitu kidogo.

Aidha imeonya juu ya tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji kwa sababu za uroho wa kupata utajiri wa haraka kufumbia macho vitendo vya rushwa katika maeneo yao ya kazi. Jambo hilo ni ni kinyume cha kanuni za uongozi wa umma ikiwamo utoaji huduma bora kwa jamii.

Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Takukuru mkoa maalum wa Kahama, Chrisantus Ndibaiukao, wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maadili iliyoanza Jumatatu (Desemba 5) ikitarajiwa kumalizika leo.

Mkuu huyo alisema suala la rushwa linapatika kwenye sekta zote na linashughulikiwa na kila mmoja ,lakini tafiti katika mkoa huo maalum , zimeonyesha kuwa malalamiko mengi na ya kukithiri kwa vitendo vya kuomba na kutoa rushwa yamo katika halmashauri , serikali za mitaa, kitengo cha ununuzi, watendaji wa kata na vijiji.Kadhalika aliitaja sekta ya afya.

Akifafanua zaidi alisema katika utoaji wa huduma baadhi ya wananchi ndiyo chanzo cha kutoa rushwa huku baadhi ya watendaji na viongozi bila woga wala kusita kupokea rushwa hiyo.

Alisema kuwa sababu kubwa ni kwa makundi yote hayo kuwa na mtazamo wa kupata huduma na utajiri kwa njia ya mkato huku baadhi ya wananchi wakitaka kuhudumiwa kiupendeleo hususani wakandarasi wanapotafuta kazi za uzabuni ndani ya serikali za mitaa.

Aliongeza kuwa wafanyabiashara hao wanatafuta zabuni hizo katika halmashauri kupitia kitengo cha manunuzi ambako hukutana na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa.

Akitoa mfano alisema wapo watoa huduma wachache hospitalini hasa madaktari na wauuguzi ambao hawapatikani kiurahisi kutokana na msongamano wa wangonjwa.

Aidha wengine hutumia upenyo huo kutaka kupata huduma kwa njia ya mkato. Alisema wazabuni wakitaka kupewa upendeleo katika katika kupata kazi kwenye halmashauri za mji na wilaya hutoa mlungula na kwamba yote hayo ni kinyume cha sheria.

Aliongeza kuwa kwa upande wa sekta ya afya, pamoja na changamoto zilizopo za upungufu wa upatikanaji wa dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati wengine hutumia upenyo huo kutaka kutoa, kuomba na kupokea rushwa.

Aidha alisema kuwa wakati umefika kwa jamii kubadilika na kuwa mstari wa mbele kupiga vita na kupambana na rushwa ,licha ya kuwa katika baadhi ya maeneo changmoto kubwa ni mila na desturi hasa katika serikali za vijiji kwa wananchi kutoa kuwa na elimu juu ya hakli yao ya msingi ya kupata huduama.

Mkuu huyo alisisitiza kuwa wakati umefika wa kufuata na kuheshimu kanuni za kutoa huduma bora,utii kwa serikali, kutoa huduma bila upendeleo,uadilifu, kuwajibika kwa umma na kuheshimu sheria.

Ujumbe wa mwaka huu kwenye maadhimisho ya Siku ya Maadili ni .’Maadili ni Nguzo Kuu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa.’

Habari Kubwa