Takukuru yataja mtuhumiwa wa sare hewa za bil. 40/-

14Sep 2017
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Takukuru yataja mtuhumiwa wa sare hewa za bil. 40/-

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemhoji kada wa Chama Cha Mapinduzi na Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa tuhuma za kutosambaza sare za Jeshi la Polisi licha ya kulipwa Sh. bilioni 40 na serikali.

Habari za uhakika kutoka Takukuru ziliiambia Nipashe jana kuwa taasisi hiyo iko katika hatua za mwisho za uchunguzi wa sakata hilo.

Sakata hilo liliibuliwa na Rais John Magufuli katikati ya mwaka jana alipokuwa akizungumza na maofisa wa Jeshi la Polisi aliowapandisha vyeo vya Naibu Kamishna wa Polisi na Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli alisema ana taarifa za rushwa ndani ya Jeshi la Polisi inayokadiriwa kuwa kati ya Sh. bilioni 40 na Sh. bilioni 60 ambazo zilipaswa kununulia sare kwa ajili ya askari polisi tangu mwaka 2015, lakini hazikununuliwa.

Habari kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya Takukuru, ambacho hakikupenda kuandikwa jina gazetini, kilisema uchunguzi wake umebaini kuwa zabuni hiyo ilitolewa kwa kampuni ya Daissy General Traders.

Aidha, chanzo hicho kilisema uchunguzi wa Takukuru pia umebaini kwamba mmiliki wa Daissy ni wa CCM na Mbunge wa zamani wa EALA (jina tunalihifadhi kwa sasa baada ya kushindwa kumpata).

Chanzo hicho kilisema kada huyo amehojiwa na maofisa wa Takukuru kama Rais alivyoelekeza na kwamba inakaribia kukamilisha uchunguzi huo kisha kumfikisha mahakamani.

Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, kujua uchunguzi wa ufisadi wa ununuzi wa sare za polisi ulipofikia na kama Mbunge huyo wa zamani wa EALA amehojiwa.

"Uchunguzi unakaribia kumalizika," alisema Misalaba. "Tumefika pazuri ila sheria hainiruhusu kueleza kile ambacho kimebainika katika uchunguzi wetu."

Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi ulibaini kuwa Daissy ilikuwa kampuni hewa.

Mbali ya kwamba ni kampuni ya mfukoni, uchunguzi huo pia ulibainika taarifa za awali zilionyesha inajihusisha na uuzaji wa vifaa vya ujenzi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, aliiambia Nipashe Januari 13, mwaka huu kuwa kampuni hiyo ni hewa kwa sababu walishindwa kubaini zilipo ofisi zake.

Rwegasira alisema awali waliambiwa Daissy General Traders ina ofisi katika makutano ya mitaa ya Uhuru na Swahili, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

WATU WALIPEANA
Kutokana na maelezo ya hayo katika anuani ya kampuni hiyo, Rwegasira alisema walifuatilia, ili kujiridhisha kama ziko sehemu hiyo, alisema, lakini walipofika hawakukuta ofisi hizo.

Jambo hilo liliwafanya wakabidhi kazi hiyo kwa Takukuru, ili ichunguze zaidi.

Katibu mkuu huyo alisema kuna uwezekano kwamba kuna watu walipeana zabuni hiyo na kampuni ambayo ni ya mfukoni isiyokuwa hata na ofisi na ndiyo maana walishindwa kuipata ilipo.

Inadaiwa kuwa kampuni hiyo iliingia mikataba na Polisi kati ya mwaka 2013-2016, lakini katika kipindi chote hicho ilishindwa kusambaza hata sare moja.

Tangu Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Tano Novemba 5, mwaka 2015, mikataba kadhaa tata imegundulika katika Jeshi la Polisi.

Mbali na mkataba huo, Polisi imechafuliwa pia na mkataba kati yake na Kampuni ya Lugumi Enterprises kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS) wenye thamani ya Sh. bilioni 37 ambao unakabiliwa na hofu ya kujaa ufisadi pia.

Katika mkataba huo ambao kwa sasa unasubiri uamuzi wa Bunge baada ya uchunguzi wa kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kampuni ya Lugumi ilitakiwa kufunga mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108.

Lakini habari za awali zilieleza kuwa ni vituo 14 tu ndivyo vilivyokuwa na mashine hizo mpaka Aprili, mwaka jana, wakati kampuni hiyo ililipwa Sh. bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote tangu 2013.

Akifungua kikao kazi cha Jeshi la Polisi katika Ukumbi wa Mikutano wa Dodoma Aprili 29, mwaka jana, Rais alilitaka kuacha kuingia mikataba yenye shaka, akigusia pia makubaliano kati yake na mwekezaji katika eneo la Oysterbay, Dar es Salaam.

Rais Magufuli alisema kama angekuwa yeye, angeendeleza eneo hilo kwa kukopa fedha za ujenzi wa jengo la kitegauchumi benki kwa kutumia hati ya eneo hilo la Kituo Kikuu cha mkoa wa kipolisi wa Kinondoni.

Habari Kubwa