Takukuru yatoa angalizo trafiki

21Jan 2019
Margaret Malisa
PWANI
Nipashe
Takukuru yatoa angalizo trafiki

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewataka madereva wanaotumia barabara za mkoa wa Pwani kutoa taarifa za rushwa wanapoombwa na askari wa usalama barabarani.

askari wa usalama barabarani akiwa kazini.picha:mtandao

Wito huo ulitolewa jana na Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani, Sadik Nombo, wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu kwa waandishi wa habari.

Nombo alisema kumekuwapo na malalamiko ya kuombwa rushwa madereva na askari, lakini wanaotoa taarifa hizo sio madereva wenyewe.

Aliwataka madereva kupiga simu au kutumia njia yoyote kufikisha taarifa katika ofisi hiyo, ili kukomesha vitendo vya rushwa vinavyolalamikiwa kila siku.

Aidha, aliwakumbusha askari wa usalama barabarani kutoa taarifa za madereva wanaowashawishi kuwapa rushwa kama walivyokubaliana kwenye kikao cha pamoja kutafuta namna ya kukomesha rushwa barabarani.

Kadhalika, alisema wamepokea malalamiko 93 yanayohusiana na vitendo vya rushwa, ambapo kati ya hayo 20 kutoka serikali za mitaa, ardhi 16, polisi 9, taasisi binafsi 9. mahakama 8, afya 4, ujenzi 4, maliasili moja, TRA moja, Tanesco 2, Sumatra moja.

Malalamiko mengine ni kutoka Dawasa 3, Maendeleo ya Jamii 3, Tasaf moja, Uvuvi moja, Viwanda moja, Ushirika moja, Mipango moja na Manunuzi moja.

Katika kipindi hicho cha miezi mitatu Takukuru ilifuatilia miradi tisa ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.4, ambapo miradi mitatu yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.3 ilitiliwa shaka na uchunguzi unafanyika.

Habari Kubwa