Takwimu wanafunzi kupata mimba Rukwa zinatisha

21Feb 2020
Nebart Msokwa
NKASI
Nipashe
Takwimu wanafunzi kupata mimba Rukwa zinatisha

TAKWIMU za wanafunzi kupata mimba katika Mkoa wa Rukwa, zinatisha ambapo zinaonyesha kuwa wanafunzi 722 wa shule za Msingi na Sekondari walipata mimba na kukatishwa masomo kati ya mwaka 2017 na  2019.

Wanafunzi wa Shule mbalimbali za Msingi na Sekondari wa Mkoa wa Rukwa wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali za kupinga ukatili wa kijinsia wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa kukabiliana na matukio ya mimba shuleni. PICHA NA NEBART MSOKWA.

Hayo yalisemwa juzi na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Bonface Kasululu, wakati wa hafla ya kuzindua Mkakati wa miaka mitano wa kukabiliana na mimba za utotoni katika Mkoa huo ambao umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mkoa huo na Shirika la Plan International kupitia Mradi wake wa Uzazi Salama.

Uzinduzi wa Mkakati huo ulifanyika katika Mji Mdogo wa Namanyere katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ambapo viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwemo wakuu wa Wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa Halmashauri, wabunge na wadau wa elimu walihudhuria.

Dk. Kasululu alisema kati ya matukio hayo ya mimba za wanafunzi, Shule za Sekondari ndizo ziliongoza kwa kuwa na matukio 551 ambayo ni sawa na asilimia 76 ya matukio yote na Shule za Msingi zilikuwa na matukio 171 ambayo ni sawa na asilimia 24.

 “Takwimu za Utafiti wa kidemografia za kati ya mwaka 2015 na 2016 zinaonyesha kuwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 19 katika Mkoa huu wanakuwa tayari ni wajawazito ama wamezaa na umri huo ndio wa kuwa shuleni,” alisema Dk. Kasululu.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, (Mwenye koti jeusi) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kitabu cha Mpango Mkakati wa kukabiliana na mimba kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa huo Mpango ambao umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mkoa huo na Shirika la Plan International kupitia Mradi wa Uzazi Salama. PICHA NA NEBART MSOKWA.

Aliongeza kuwa chanzo cha watoto hao kupata mimba za utotoni ni uwajibikaji mdogo wa wazazi na walezi, viongozi pamoja na jamii za watu wa Mkoa huo katika masuala ya ulinzi wa watoto wa kike ambao wako katika hatari zaidi.

Alizitaja sababu zingine kuwa ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu Sheria zinazosimamia masuala ya mahusiano ya watoto, ukatili wa kijinsia, shinikizo rika, idadi ndogo ya shule za bweni hali inayosababisha wanafunzi kusafiri umbali mrefu na kukosekana kwa chakula shuleni.

Habari Kubwa