Tamisemi, RC waunda tume kuchunguza ufisadi mil. 730/-

05Jan 2017
Nebart Msokwa
Kyele
Nipashe
Tamisemi, RC waunda tume kuchunguza ufisadi mil. 730/-

UPOTEVU wa zaidi ya Sh. milioni 733 za maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, umeizindua serikali na kuunda tume mbili kuchunguza sakata hilo.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makalla.

Tume zilizoundwa ni za watu watatu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambayo pia ina watu watatu. Kila tume itafanya kazi kwa wakati wake.

Akizungumza juzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa na lengo la kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, alisema Tamisemi na ofisi yake wamelazimika kuunda tume kuchunguza ubadhirifu huo.

Makala alisema wajumbe wa tume aliyounda wanatoka nje na Wilaya ya Kyela na mmoja kutoka mkoani Rukwa ili kuifanya kuwa huru zaidi.

Aliwataja watu wanaounda tume hiyo kuwa ni Constantine Mushi, kutoka katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mosses Mashaka ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Rungwe na Mhandisi Emmy George kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa.

Aliwataja pia wajumbe wa tume iliyoundwa na Tamisemi kuwa ni Ally Rashid, Subilaga Mwaisela na Mussa Kiloka.

Makala alisema katika kila mkutano aliofanya na wananchi wa wilaya hiyo, suala la upotevu wa fedha za halmashauri lilikuwa linaibuka hivyo akaona kuna sababu ya kuunda tume huru.

“Kila nilipofanya mikutano na wananchi wa wilaya nimekuwa nikiulizwa maswali na wananchi ambayo ni ya menejimenti ya halmashauri.

Sasa naheshimu sana kazi mliyoifanya kama halmashauri ya kuunda timu ya kuchunguza ambayo ilikuja na majibu kwamba hakuna upotevu. Sasa tunataka kujiridhisha,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Tuna taarifa kuwa kuna mgawanyiko wa madiwani hapa. Wengine wakikubaliana na tume yenu na wengine wakapinga ndiyo maana nikaamua kuunda tume huru ambayo mjumbe mmoja anatoka nje ya mkoa, lakini wizara nayo imeunda tume hivyo tusubiri majibu.”

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Dk. Hanter Mwakifuna, aliishukuru serikali kwa kuingilia kati sakata hilo linaloonyesha kusababisha mpasuko wa madiwani na wananchi kukosa imani na serikali.

Alisema taarifa zote walizozifanyia kazi walizipata kupitia kwenye vikao mbalimbali vya Baraza na kwamba walikubaliana kwa pamoja na pale waliposhindwa kukubaliana walipiga kura kama kanuni za baraza zinavyoelekeza.

Alisema majibu ya tume hizo mbili ambazo zote ni huru ndiyo yatakayoleta suluhu na utengamano wa madiwani pamoja na watumishi wengine wa Halmashauri hiyo.

Hata hivyo, alisema endapo kilichokuwa kimeamuliwa na Halmashauri hiyo kitaonekana kuwa ni sahihi watapongezana, lakini kama kitaonekana si sahihi, wote waliosababisha tatizo hilo watachukuliwa hatua kali.

Agosti, mwaka jana, ziliibuka taarifa ndani ya vikao vya halmashauri hiyo kuwa fedha hizo za maendeleo zimeliwa, hali iliyosababisha Baraza la Madiwani kuwasimamisha watumishi wawili wa idara ya fedha ili kupisha uchunguzi.

Watumishi waliosimamishwa ni pamoja na Arapha Baraza ambaye ni Mweka Hazina wa Halmashauri na Salome Lyimo, ambaye ni Ofisa Ununuzi wa Halmashauri

Halmashauri hiyo iliunda tume ambayo ilifanya uchunguzi wa matumizi ya fedha hizo na kubaini kuwa hakuna upotevu wowote, hivyo kupendekeza watumishi hao kurejeshwa kazini, hali iliyozua mpasuko miongoni mwa madiwani.

Habari Kubwa