TAMISEMI yajivunia kupungua utapeli

21Nov 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
TAMISEMI yajivunia kupungua utapeli

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imesema kuanzishwa kwa kituo cha huduma kwa wateja katika ofisi hiyo kumepunguza matukio ya utapeli, huku watumishi wakiagizwa kushughulikia kero ndani ya siku tatu na si zaidi.

Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Joseph Nyamhanga, aliyasema hayo jana alipotembelea kituo hicho kilichoanzishwa Agosti 6, mwaka huu.
 
Alisema kabla ya kuanzishwa kwa kituo hicho, kulikuwa na matukio mengi ya utapeli hususani kwa walimu wanaofuatilia uhamisho ikiwamo kutolewa kwa barua feki za uhamisho.
 
“Watumishi wengi wetu ni walimu na hawa ndio walikuwa waathirika wakubwa wa tatizo hili na ilifikia hadi kugushiwa barua za uhamisho ambazo walikuwa wakizigharamia, lakini kwa sasa hali hiyo haipo,” alisema.
 
Aidha, Nyamhanga aliagiza wakuu wa idara za wizara hiyo kushughulikia kero na hoja za wateja wa wizara hiyo ndani ya siku tatu na si zaidi ya hapo.
 
Alitoa rai kwa watumishi na Watanzania kwa ujumla kutumia kituo hicho jambo ambalo litasaidia kuwaondolea kero ya kusafiri na gharama.
 
Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Antelma Mtemahanji, alisema ndani ya miezi minne tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, hoja na matatizo ya wateja yameshughulikiwa kwa asilimia 99 huku asilimia moja ikiwa katika hatua za kushughulikiwa.
 
Alisema tangu kuanza kituo hicho, wamepokea simu 15,886, wateja waliosajiliwa ni 5,571 na hoja zilizosajiliwa ni 5,571.
 
Mtemahanji alisema kabla ya kuanzishwa kwa kituo, walikuwa wanapokea wageni wenye shida mbalimbali kutoka watu 87 hadi 129 kwa siku lakini kwa sasa idadi hiyo imepungua na hawazidi watu 20.
 
Alisema baadhi ya hoja ambazo zimeshughulikiwa ni uhamisho kwa walimu, stahiki za watumishi ikiwa ni kupanda daraja au kubadilishiwa mshahara na kutaka kupata ufafanuzi wa mifumo na ajira.
 

Habari Kubwa