TAMWA yafagilia uteuzi mawaziri wanawake 2

14Sep 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
TAMWA yafagilia uteuzi mawaziri wanawake 2

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuteua wanawake wawili katika Baraza la Mawaziri, uteuzi uliofanyika juzi.

Katika uteuzi huo, Rais Samia alimteua Dk.Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Dk. Stergomena Tax, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

“TAMWA tunampongeza Rais Samia, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kumteua mwanamke kushika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Uteuzi huo unaonyesha dhahiri kuwa wanawake wanaaminika na wana uwezo wa kuleta mabadiliko katika nyanja zote, kisiasa, kiuchumi na kijamii, uteuzi huu unafanya idadi ya mawaziri wanawake kufikia saba kutoka watano walioteuliwa awali” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben.

Alisema TAMWA wanaamini kuwa, ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ndiyo nguzo muhimu ya kuleta usawa na ni chanzo cha kuleta mabadiliko chanya katika jamii, ambayo yanatokana na usawa, haki na uwajibikaji.

“Rais Samia, ameonyesha lile ambalo lilidhaniwa haliwezekani kwa kuwaweka mawaziri wanawake katika wizara nyeti kama ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, pia kwa kuendelea kuteua mawaziri wanawake, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na makatibu tawala,” alisema Dk. Reuben.

Hakika Rais amevunja dhana ya kuwa wanaume pekee ndiyo wenye uwezo wa kushika wizara hii, na kwa hili tunategemea Dk. Tax hatatuangusha, bali atasimamia vyema nafasi hiyo na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika masuala ya ulinzi na usalama, kwa kuwa ana uwezo na upeo.”

Pia, TAMWA ilimpongeza Rais Samia kwa kusikiliza kilio cha wanahabari kwa kuunganisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na ile ya Teknolojia ya Mawasiliano, kuwa moja.

“Hatua hiyo itasaidia wadau wa habari kufanya kazi kwa ufanisi na wepesi zaidi kuliko hapo awali.Tunaamini kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi na katika ngazi za uamuzi ndicho chanzo cha haki, usawa na uwajibikaji na maendeleo ya nchi,” alisema Dk. Reuben.