TAMWA yalaani kushamiri matukio ukatili kwa watoto

21May 2022
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
TAMWA yalaani kushamiri matukio ukatili kwa watoto

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), kimelaani matukio ya ukatili wanayoendelea kufanyiwa watoto katika maeneo mbalimbali nchini na kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya sera na sheria za kuwalinda.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben, aliyaeleza hayo jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kusema kuwa kunzia Januari hadi Mei mwaka huu matukio matano yaliripotiwa.

Alitaja aina ya matukio hayo kuwa ni lililotokea mkoani Katavi la mwalimu wa mafundisho ya dini ya kikristo, Joseph John kuwalawiti watoto wanne.

Alisema lingine ni mkazi wa Iringa aliyedaiwa kumlawiti mtoto wake wa kambo, watoto 14 kulawiti watoto wenzao 14 wa kiume na tukio la mwalimu wa madrasa Jumanne Ikungi, mkazi wa Arusha kuwalawiti wanafunzi 22 wa Shule ya Msingi Mkonoo.

“Kwa matukio haya yaliyoripotiwa kati ya Januari hadi Mei, inatosha kusema kuwa watoto wetu hawapo salama na TAMWA tunalazimika kusema, watoto hawa hawana pa kukimbilia.

“Mwenendo huu wa matukio ya ubakaji na ulawiti wa watoto tena na walimu, viongozi wa dini, wazazi na walezi, unadhihirisha kuwa tatizo hili bado ni kubwa nchini na linahitaji uamuzi mgumu kutoka kwa watunga sera wetu,” alisema Dk. Reuben.

Alisema kuwa, pamoja na wadau wengine wa masuala ya jinsia wamekuwa wakiimba na kuitaka jamii kuzuia ukatili kwa miaka zaidi ya 30 hasa wakililia mabadiliko ya sera, sheria na kutoa elimu kwa jamii.

Aidha, alisema taarifa za makosa ya ukatili wa jinsia na unyanyasaji zilizotolewa na Jeshi la Polisi katika chama hicho mwaka jana, zilionyesha mikoa ya kipolisi iliyoongoza kwa ukatili dhidi ya watoto ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Ilala 489.

Aliongeza kuwa, makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ya matukio ni ya ubakaji 5,899, kumpa mimba mwanafunzi 1,677, ulawiti 1,114, kumzorotesha mwanafunzi masomo 790 na shambulio 350.

Alisema utafiti uliotolewa hivi karibuni na taasisi ya Haki Elimu, unaonyesha kuwa watoto wengi hawafundishwi elimu ya afya ya uzazi, lakini zaidi sasa walimu nao wanaogopa kufundisha wanafunzi mada hizo.

Habari Kubwa