Tamwa yampongeza JPM kukemea mimba wanafunzi

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tamwa yampongeza JPM kukemea mimba wanafunzi

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimempongeza Rais John Magufuli, kwa kuzungumzia kwa uwazi na kukemea hadharani suala la ongezeko la mimba kwa wanafunzi mkoani Rukwa.

Rais John Magufuli, picha mtandao

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Rose Ruben, ilisema chama hicho miongoni mwa malengo yake ni kupunguza mimba za utotoni na unyanyasaji wa kijinsia.

Alisema mimba za utotoni zinaitia hasara serikali inayotoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya elimu bure, shule za msingi na sekondari, na kwamba mimba hizo ndicho chanzo cha vifo vya uzazi na maradhi ikiwamo Ukimwi.

Kwa mujibu wa Reuben, taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa baadhi ya wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi ni walimu, polisi na madereva bodaboda wasiofuata maadili.

"Wakati makundi hayo yanaaminiwa katika kuwapa ulinzi wanafunzi. Kama Rais Magufuli alivyosisitiza, Tamwa inawasihi wazazi na walezi wawafundishe watoto kuepuka vitendo vya ngono na tunaziomba taasisi za dini kuwaelimisha watoto wa kike kujiepusha na vitendo hivyo," alisema.

Aliwaomba viongozi wa dini watoe mawaidha ya kuwakanya wanaume wanaolaghai wanafunzi.

Rais Magufuli ambaye alikuwa ziarani mkoani Rukwa alisema kwa takwimu alizopata kulikuwa na wanafunzi 229 waliopata mimba mkoani humo mwaka jana pekee.

Habari Kubwa