TAMWA yamshukuru Rais Samia waliopata mimba kurejea shuleni

14May 2022
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
TAMWA yamshukuru Rais Samia waliopata mimba kurejea shuleni

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuridhia watoto wa kike waliopata ujauzito kurejea shuleni kuendelea na masomo.

rais samia suluhu hassan.

Mkurugenzi Mtendaji TAMWA, Dk. Rose Reuben, alitoa pongezi hizo jana mkoani Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 10 ya Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambayo Rais Samia alikuwa mgeni rasmi.

"Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita, mwaka jana iliridhia na kuruhusu watoto wa kike ambao wamepata ujauzito baada ya kujifungua kurejea tena shuleni kuendelea na masomo, hili ni jambo zuri," alisema Dk. Reuben.

Alisema mimba za utotoni zimekuwa zikitokea kwa sababu nyingi ikiwamo ndoa za utotoni, malezi mabaya kwa watoto wa kike, ubakaji ama makosa ya kibinadamu.

Dk. Reuben alisema katika kipindi cha miaka 10 ya THDRC, TAMWA imeendelea kupinga kwa kiwango kikubwa ukatili wa kijinsia kwa wanawake, wasichana, watoto na wanaume.

"Wanawake watu wazima na wenyewe wana haki zao na hata wanawake wazee wana stahiki zao na wanapokuwa na haki zao maana yake wanahitaji kulindwa na kutetewa," alisema.

Katika kipindi hicho, alisema  TAMWA imeendesha kampeni ya kupinga mauaji ya wanawake wazee ambayo yalifanyika mkoani Shinyanga na maeneo mengine kwa kuwatuhumu kufanya uchawi.

Dk. Reuben alisema suala la mila potofu ni kampeni waliyoianzisha kwa ajili ya kuzuia ukatili kwa wanawake ambao wanafanyiwa.

Alisema pia walifanya kampeni ya kutungwa sera na adhabu kali kwa wale wanaotekeleza mila potofu ikiwamo kuozesha watoto katika umri mdogo, ubakaji na mimba za utotoni.

Naye Mraribu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, aliiomba serikali kuwapo na sheria au sera za kuwatambua watetezi wa haki za binadamu.

Habari Kubwa