Tamwa yapata mkurugenzi mpya

12Jan 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Tamwa yapata mkurugenzi mpya

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa),kimepata Mkurugenzi Mtendaji mpya, Rose Ruben, baada ya aliyekuwapo, Edda Sanga, kumaliza muda wake wa miaka mitatu.

Kaimu Mwenyekiti wa Tamwa,Judica Losai (Kushoto) akikabidhi katiba Kwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Tamwa,Rose Ruben

Akimtambulisha jana mkurugenzi mpya kwa waandishi wa habari, wanachama na wafanyakazi wa Tamwa, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Judica Losai, alisema kupatikana kwa mkurugenzi huyo kulitokana na mchakato mrefu na kwamba kubadilishana uongozi umekuwa utamaduni wa muda mrefu.
 
Akizungumza kabla ya kukabidhi nyaraka mbalimbali, Sanga aliwashukuru waandishi wa habari na vyombo vya habari kwa ujumla kwa kupaza sauti za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, kiasi cha kufikia kwenye hatua ya kuridhisha kwa watu wengi kuwa na uelewa.
 
“Kazi kubwa ya Tamwa ni ukatili wa kijinsia. Naomba mwendelee kushirikiana na Tamwa kukomesha ndoa za utotoni, ulawiti na ubakaji unaoendelea kwenye jamii yetu,” alisema.
 
Aidha, alisema wakati Tamwa inaanzishwa watu wengi hawakuwa na uelewa wa umuhimu wa wanawake katika mchakato wa maendeleo, lakini kulikuwa na wanachama jasiri ambao walipigania kwa kiasi kikubwa kuhakikisha nafasi ya mwanamke inatambuliwa na kuthaminiwa.
 
“Kwa sasa kuna mabadiliko makubwa watu wako tayari kuzungumza kuhusu matukio ya ukatili tofauti na miaka 1987 wakati Tamwa inaanzishwa,tunafurahi serikali inaunga mkono harakati hizi na sasa mafanikio yanaonekana na watu wanauelewa,” alisema
 
“Tulitaka kupata waandishi wa habari wengi wanawake kwenu vyombo vya habari ili habari zetu ziandikwe kwa jicho la jinsia na kupaza sauti jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alibainisha.
 
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, changamoto kubwa iko kwenye kuharibu ushahidi kunakofanywa na polisi na madaktari hasa kwenye kesi za ulawiti na ubakaji wa watoto ambao unaendelea na kesi zinaharibiwa huku wazazi na walezi wakikubali kumaliza kesi nyumbani na hivyo kuwathiri kisaikolojia na kimaisha watoto hao.
 
Naye Ruben alisema ukatili wa kijinsia hakipendezi na kuna sheria na taratibu za kushughulika na wanaofanya jambo hilo.
 
“Nawasihi waandishi muendelee kuandika mambo yanayohusu ukatili wa kijinsia ili kuwa na Tanzania inayojali haki ya mtoto wa kike ili kuwa na taifa imara lenye watu wanaofanyakazi na hawajakumbwa na ukatili wa kijinsia unaoathiri saikolojia,” alisema.
 
Alisema kila mtu atatambua mtoto na mwanamke ana haki ya kuishi na kufurahia maisha na ikifikia hapo itawezekana kushiriki katika uchumi wa viwanda.
 
Naye mwanachama mwanzilishi wa Tamwa, Fatima Aloo, alisema Tamwa ilipitia changamoto mbalimbali katika kipigania haki za watoto na ,wanawake,lakini iliendelea kusimama kuhakikisha jamii inaitwa uelewa kwa kutumia vyombo vya habari.

Habari Kubwa