TAMWA yazindua kampeni ya kuzuia ukatili mitandoni

17Apr 2021
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
TAMWA yazindua kampeni ya kuzuia ukatili mitandoni

CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kimezindua kampeni ya ‘Zuia Ukatili Mtandaoni’ ambayo inalenga kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike mitandaoni.

Kadhalika, kimetoa wito kwa serikali na asasi za kiraia kuzungumzia madhara ya vitendo vya ukatili wa mitandao na kutoa elimu kwa jamii ili kuondoa tatizo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Sylvia Daulinge, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben, alisema ukatili wa mtandao umekuwa ukiwaathiri zaidi watoto wa kike na wanawake kutokana na namna ya makuzi na desturi za jamii.

Daulinge alisema takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa mtandao mpaka mwaka 2017 watumiaji waliongezeka kwa asilimia 16 na kufikia idadi ya milioni 23.

"Tumeona mara kadhaa video za utupu za wanawake, watoto wakike zikisambazwa katika mitandao hiyo. Tumeshuhudia matukio ya video za ngono za wanawake zikisambazwa kwa makusudi kabisa, huu ni udhalilishaji unaofanyika kwa njia ya mtandao,"alisema.

Daulinge alisema udhalilishaji huo una madhara kisaikolojia na kusababisha watu kuathirika kisaikolojia na wengine kujiua au kupoteza mwelekeo katika maisha.

"Bado udhalilishaji huu unaendelea pengine ni waathirika kutoifahamu sheria hii au kuona aibu katika kutafuta haki au hofu ya kudhalilika zaidi kesi itakapopelekwa mahakamani," alisema.

Alisema TAMWA haikubali udhalilishaji huo, ni muhimu wananchi wakatambua sheria zinawalinda, kwamba kuna adhabu kwa wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya ikiwamo faini ya Sh. milioni tano au kifungo kisichopungua miezi 12 au kwa vyote kwa pamoja.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Dawati la Jinsia na Watoto Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Leah Mbunda, alisema kampeni hiyo itasaidia kuleta chachu katika jamii katika kuwoangezea wananchi uelewa.

Alisema wapo ambao wanadhalilishwa katika mitandao ya kijamii wanakaa kimya na wengine kuona aibu.

Habari Kubwa