TANAPA yahamashisha Watanzania kutembelea hifadhi

08Dec 2021
Maulid Mmbaga
Nipashe
TANAPA yahamashisha Watanzania kutembelea hifadhi

UONGOZI wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Kanda ya Mashariki umetoa wito kwa watanzani katika msimu wa sikukuu kutembelea hifadhi mbalimbali zilizopo nchini ili kupata fursa ya kujifunza na kuona vivutio tofauti vilivyomo.

Akizungumza Leo Jijini Dar es Salaam, Kamishna Mwandanizi wa Uhifadhi Kanda ya Mashariki (TANAPA) Steria Ndaga amesema, kila mwaka mwezi Desemba wanapata idadi kubwa ya watalii wa ndani, jambo linalowasukuma kuendelea kutoa hamasa kwa watanzania kutembelea hifadhi hasa za kanda ya mashariki.

Amesema katika Hifadhi za Taifa Mikumi, Milima ya Udzungwa, Saadani, Nyerere, Nyumba ya Makumbusho ya Mwalimu Nyerere na Kituo cha Utumwa Caravan Serai – Bagamoyo, zinamchanganyiko wa vivutio na shuhuli za utalii za kipekee zinazowapendeza watalii wengi wanaotembelea maeneo hayo.

“Katika kuadhimisha miaka 60 ya uhuru na kuelekea msimu wa sikukuu tunawakaribisha watanzania tupate nafasi ya kupumzika katika mapori yetu ya hifadhi, kaulimbiu yetu ni Desemba 2021 Bata lote Porini, tukiwa na maana kwamba vijana, wakubwa na wazee tutembelee tukafurahie maisha ya porini.

“Watalii watakaotembelea hifadhi hizo watapata fursa ya kufanya shughulI za kitalii kama kuangalia wanyama kwa nyakati za mchana na usiku, utalii wa ufukweni, kupanda milima, uwepo wa maporomoko ya maji, kujifunza historia ya mambo ya kale na za muasisi wetu hayati Mwl Nyerere katika harakati za kugombania uhuru,” amesema Steria.

Ameongeza kuwa upekee mwingine wa hifadhi hizo ni uwepo wake katika eneo mkakati kwani zimepakana na miji mikubwa kama Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Tanga, Iringa na Zanzibar na zinafikika kirahisi, pia kwa watalii wanaopenda kukaa zaidi ya siku moja malazi yanapatikana ndani ya hifadhi.

Aidha katika msimu huu wametoa ofa kwa wakazi wa Dar es Salaa kwa kuandaa safari za kuta na kulala kwenda hifadhi za taifa Mikumi, Milima Udzungwa, Saadani na Nyerere, na watakaopenda kutembelea wenyewe gharama za kiingilio ni sh 5000 kwa mtu mmoja.

“Kuanzia Disemba 6 hadi 12 tutakuwepo jijini Dar es Salaam na tumeweka vituo katika maeneo mbalimbali kama Airport Terminal 2, Shoppers Plaza Mbezi Beach, Palm Village na Mlimani City tutakuwa tukitoa taarifa sahihi jinsi ya kutembelea hifadhi za taifa, na ratiba za safari zimewekwa katika mitandao yetu ya kijamii,” alisema Steria.

Pia amebainisha kuwa gharama za matembezi katika Hifadhi ya Mikumi kwa siku ni Sh 70,000 siku mbili na usiku 160,000, Saadani siku moja 65,000 siku mbili 155,000, Nyerere siku moja 75,000 siku mbili 175,000 na Udzungwa siku mbili 185,000.

Habari Kubwa