Tanesco ‘yakwaa kisiki’

24Nov 2016
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Tanesco ‘yakwaa kisiki’

WADAU wa umeme nchini jana walipinga maombi ya Shirika la Umeme (Tanesco) ya kupandisha bei ya umeme kwa maelezo kwamba sababu zilizotolewa hazijitoshelezi.

Tanesco iliomba kuongeza bei ya umeme hadi kufikia asilimia 18.19 kuanzia Januari, mwakani.

Wakizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Umeme na Maji (Ewura), wadau hao walisema sababu za Tanesco kuomba kupandisha bei ya umeme huo hazina mashiko na kuwataka warudi wakajipange upya.

Mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali kujadili ombi hilo.

Walisema wanashangaa kuona Tanesco inataka kupandisha kiwango hicho kikubwa cha bei ya umeme huku wakiwa hawana sababu za msingi za kufanya hivyo.

Baadhi ya vyombo vilivyoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Baraza la Ushauri la Serikali lililowakilishwa na Kaimu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Amani Mafuru.

Mafuru alisema baada ya kupitia sababu za Tanesco za kuomba kupandisha bei hiyo, lilibaini kwamba sababu hizo hazijitoshelezi.
Alisema maombi hayo yalitakiwa kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja tofauti na utaratibu uliowekwa na Ewura wa kupitisha bei za miaka mitatu mitatu.

"Baraza limeishauri Ewura iwatake Tanesco kutoa maelezo na sababu zilizowafanya washindwe kuwasilisha maombi ya bei ya miaka mitatu kama utaratibu ulivyo, waeleze bei za miaka mingine inayofuata baada ya bei hizi kupitishwa ambazo zitaishia Desemba, 2017 zitakuwaje,” alisema Mafuru.

Pia alisema kitendo cha Tanesco kushusha na kupandisha bei katika kipindi kifupi, siyo sahihi kiuchumi na haileti tija kwa wananchi na wafanyabiashara na kunazifanya bei hizo kuwa zisizotabirika.

Alisema andapo Tanesco watakubaliwa maombi yao, wateja wake watalazimika kulipa gharama zaidi kwa kupata nishati ya umeme na itachangia kuongeza ugumu wa maisha.

Aidha, Mafuru alisema Tanesco imeshindwa kutoa uchambuzi wa gharama inazotumia katika kuzalisha, jambo ambalo ingekuwa rahisi kwa wachambuzi kubaini hasara za shirika zinatokana na nini.

Mafuru aliishauri Ewura kuwataka Tanesco kuwasilisha taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ili kuwawezesha wadau na wachambuzi kujua hali halisi ya utendaji wa shirika.

Kwa upande wake, Baraza la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura CCC), kupitia kwa Kaimu Mwenyekiti wake, Thomas Mnunguli, alisema kabla ya Tanesco kuomba kuongeza bei ya umeme, ilipaswa kuwasilisha serikalini na Ewura mkakati wa kukusanya madeni toka kwa serikali na taasisi zake wanazozidai.

Kwa mujibu wa Tanesco, deni la shirika hilo limeongezeka kutoka Sh. bilioni 699.57 Desemba, mwaka jana hadi kufikia Sh. bilioni 794.48 mwezi Septemba,huku kati ya madeni hayo taasisi za serikali zikidaiwa Sh. bilioni 148.

Mnunguli alisema kabla ya kuongeza bei hiyo, shirika linapaswa kukusanya madeni yote kutoka kwa wadaiwa sugu ikiwamo kuwakatia umeme na kutoa sababu za kushindwa kukusanya madeni hayo.

Kwa upande wake, Cyprian Mtweve, kutoka Kiwanda cha Saruji cha Tanga, alisema sababu za Tanesco hazina mashiko kwa sababu bei ya mafuta katika soko la dunia bado haijabadilika, na thamani ya Shilingi nayo iko vizuri.

Mtweve aliitaka Tanesco irudi na kwenda kutafakari sababu nyingine zitakazoeleweka.

Kwa mujibu wa Ewura, maoni hayo ya kujadili ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme, yanaendelea kupokelewa hadi kesho.

Habari Kubwa