Tanesco Shinyanga waomba radhi kukatika kwa umeme

24Mar 2020
Marco Maduhu
Shinyanga.
Nipashe
Tanesco Shinyanga waomba radhi kukatika kwa umeme

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoani Shinyanga, limeomba radhi wateja wake kutokana na tatizo la kukatika katika kwa umeme mara kwa mara, kila ifikapo saa moja na nusu jioni na kuwa sababishia usumbufu.

Afisa uhusiano na wateja kutoka Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Shinyanga Sarah Libogoma akizungumza na waandishi wa habari na kuomba radhi kwa wateja tatizo la kukatika katika kwa umeme mkoani humo.

Radhi hiyo imeombwa leo na  Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja, kutoka shirika hilo mkoa wa Shinyanga, Sarah Libogoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema shirika hilo linaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa kukatika katika kwa umeme mkoani humo, na kubainisha tatizo hilo lilitokana na hitilafu kwenye miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme kutoka Kidatu kwenda Iringa, ambapo mto Ruaha ulijaa maji na kusababisha nyaya za umeme kugusa maji.

“Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga, tunaomba radhi sana wateja wetu kutokana na tatizo la kukatika katika kwa umeme ndani ya muda wa siku tano, ambapo kwenye njia zetu za kusafirisha umeme zinazopita kando ya mto Ruaha zilipata hitilafu sababu ya maji kujaa na kugusa nyaya za umeme,” amesema Libogoma.

“Tatizo hili la kukatika kati kwa umeme halitaweza kujitokeza tena, sababu mafundi wetu wameshalifanyia kazi, na sisi Tanesco mkoani Shinyanga tutaendelea koboresha huduma kwa wateja wetu, pamoja na kuondoa nguzo za umeme ambazo zimesha chakaa, na kukata miti ambayo ipo karibu na nyaya za umeme,” ameongeza

Aidha amesema kutokana na kukatika kwa umeme hakuna taarifa yoyote iliyotolewa ya madhara kwa wananchi, huku akitoa wito pale watakapoona kunatatizo la umeme watoe taarifa mapema, pamoja na kutunza miundombinu ya Shirika hilo la umeme na kuto iharibu.

Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga akiwamo Jackson Mapolu mkazi wa Ndala, amesema kukatika huko kwa umeme majira hayo ya saa moja na nusu jioni na kurudi mida ya saa tatu usiku, ilikuwa kero kwao, pamoja na kukosa kuangalia taarifa ya habari saa 2 usiku hasa kupata taarifa za virusi vya corona.

Habari Kubwa