Akizungumza jana wakati wa kukabidhi kisima hicho, Mkurugenzi wa Fedha wa TANESCO, Renata Ndege aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Maharage Chande alisema licha ya kwamba kazi kubwa ya shirika ni kusambaza umeme lakini pia wanaijali jamii kwa kuwa wanatambua wanategemea.
“Tumekuja kukabidhi kisima cha maji chenye thamani ya Sh. milioni 14, ambacho kitawasadia wanafunzi na wanakijiji wa Nyani kuondokana na changamoto ya upatikanaji maji safi na salama waliyokuwa nayo kwa muda mrefu,”alisema.
Pamoja na kukabidhi kisima hicho pia, walipanda miti 100 kwenye eneo la Shule ya msingi Nyani, ikiwa ni mkakati wa TANESCO kutunza mazingira kwa faida ya wote.
“Sote tunafahamu umuhimu wa miti katika kuleta mvua ambazo kwa kiwango kikubwa huchangia uwepo wa maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme nchini, hivyo tunachokifanya leo kina uhusiano wa moja kwa moja na uwepo wa umeme wa uhakika nchini,” alifafanua Ndege.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, matukio yote yanayofanyika ni muendelezo kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8 mwaka huu.
“Ndio sababu leo tumekuja wanawake wa TANESCO, hususan wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kutekeleza shughuli hizi,” aliongezea.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mradi huo, Diwani wa Kata ya Mfizi, Yadhamicas Nghondo aliishukuru TANESCO kwa kuwambukuka wanafunzi na wanancho hao ambao walikuwa hawana hudumaya maji safi na salama.
Alisema wananchi walikuwa wanatafuta maji Mto Ruvu umbali wa kilomita tano jambo ambalo lilikuwa ni hatari hasa kwa wanawake na wasichana huku muda mwingi wa uzalishaji ukipotea.
“Ni kweli kuwa shughuli za TANESCO ni kusambaza umeme na kuangazia maisha ya watanzania, lakini wamekuja kutuangazia maisha yetu kwa kutulekea maji ambayo ni uhai kwetu, tunaahidi kutunza mradi huu ili uwe endelevu,”alisema.
Huu ni mradi mwingine wilayani humo baada ya ule wa mwaka 2019 na 2020 TANESCO kupitia wafanyakazi wa mikoa hiyo walijenga nyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na choo cha matundu sita kwa shule hiyo.
Alisema jitihada hizo zilisaidia kuongeza ufahulu kwa wanafunzi wa shule hiyo kwa zaidi ya asilimia 80 mwaka jana huku shirika hilo likiahidi kuendelea kuboresha mazingira ya shule hiyo kwa kupaka rangi, sakafu na maeneo mengine.