TANESCO yakamilisha umeme treni ya kisasa

27Feb 2021
Joseph Mwendapole
Morogoro
Nipashe
TANESCO yakamilisha umeme treni ya kisasa

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limekamilisha ujenzi wa vituo vinne vya kusafirisha na kupoza umeme utakaotumika kwa ajili ya treni ya kisasa (SGR) kwa asilimia 99 na kazi iliyobaki ni kuunganisha nishati hiyo tu.

Hayo yalisemwa jana mjini Morogoro na Meneja Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi wa Umeme wa SGR kutoka Kinyerezi hadi Kingoruwila mkoani hapa, Mhandisi Albano Sembua.

Alikuwa akizungumza na wahariri waandamizi na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini waliotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

Alisema ujenzi wa mradi huo una urefu wa kilometa 159 kuanzia Kinyerezi, Dar es Salaam hadi Kingorwila mkoani Morogoro ukiwa na nguzo 462 na zote zimeshajengwa pamoja na kuvuta nyaya.

Aliwaambia wahariri hao kuwa mradi ulianza Januari, 2019 na umekamilika mwaka jana.

“Mradi huu umegawanyika sehemu kuu mbili, kwanza kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi hadi hapa Kingorwila na kazi ya pili ni kupanua kituo cha umeme cha Kinyerezi kazi zote mbili zimekamilika.

“Ujenzi umefikia asilimia 99 na  unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na fedha zilizotumika ni Sh bilioni 71.1 na mpaka sasa hivi na tumeshafanya malipo kwa mkandarasi Sh. bilioni 60 ambazo ni sawa na asilimia 84," alisema Mhandisi Sembua.

Pia alisema kinachosubiriwa kwa sasa ni kuunganisha umeme huo katika vituo vinne vya umeme wa SGR ambavyo vimejengwa Pugu, Ruvu, Kidugalo na Kingorwila.

"Kazi ya kuunganisha umeme itaanza wiki ijayo na umeme ambao utazalishwa kwa ajili ya SGR ni wa uhakika na hautakatika hata siku moja kwani vyanzo vyake ni vya uhakika na maalum kwa ajili ya mradi huu tu na kuna laini ya umeme inayotoka Kinyerezi na kuna laini ya umeme ya Morogoro kuja SGR,” alisema.

"Kwa hiyo ikitokea laini ya Kinyerezi imeleta hitilafu basi laini ya Morogoro itatumika, pia tunayo laini nyingine ya  umeme wa Ubungo ambayo nayo imepita Kinyerezi kuja hapa kwa hiyo tunaweza kutumia umeme wa Ubungo,"alifafanua.

Kuhusu faida za mradi huo wa SGR, alisema TANESCO wamepata mteja mkubwa ambaye ni Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambaye atahitaji umeme kwa ajili ya treni hiyo ya kisasa inayotumia umeme.

Kuhusu uwezo wa umeme unaozalishwa kwa ajili ya SGR, Mhandisi Sembua alisema laini hiyo inauwezo wa kubeba umeme wa megawati 500 lakini mahitaji ya sasa ya TRC ni megawati 70.

Aliongeza kuwa vituo vinne ambavyo wamevijenga kazi yake kubwa ni kupunguza umeme unatoka Kinyerezi ambao unakuwa kilovoti 220, hivyo lazima upungue hadi kilovoti 27.5 ambao ndio unaingizwa kwenye mfumo wa SGR.

"Mradi huu ni maalum kwa ajili ya reli ya kisasa na tangu Kinyerezi hadi Kinguruwila na hawajaunganishia mteja mwingine zaidi ya TRC peke yake kwa ajili ya reli tu,"alisema na kuongeza.

"Sababu ya kuzalisha megawati 500 kwa ajili ya SGR, tunaamini huko mbele ya safari TRC wanaweza kuamua kuongeza miudombinu kwa ajili ya treni ya kisasa, hivyo tumeamua kuwawekea mapema," alisema

Habari Kubwa