Tanesco yawaangukia wananchi ulinzi miundombinu ya umeme

27Jan 2019
Joseph Mwendapole
Arusha
Nipashe Jumapili
Tanesco yawaangukia wananchi ulinzi miundombinu ya umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limewahimiza Watanzania kuwa na uzalendo kwa kuwafichua watu wanaohujumu miundombinu ya shirika hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Wito huo ulitolewa jana na Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji, wakati wa ziara ya wahariri na waandishi wa habari kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo mkoani Arusha.

 

Akizungumza kwenye kituo cha kupoza umeme cha Njiro, Muhaji  alisema wananchi ni wanufaika wakubwa wa nishati inayozalishwa, hivyo kwa kuwa wanakaa jirani na miundombinu hiyo, watoe taarifa kila wanapoona mtu anataka kuihujumu.

 

 

“Tunawaomba wananchi wakimwona mtu yeyote anataka kuharibu miundombinu ya shirika, atoe taarifa mapema ili wahusika wachukuliwe hatua. Miundombinu hii imeigharimu nchi fedha nyingi, hivyo lazima tuilinde kwa gharama yoyote kwa  manufaa yetu sote,” alisema.

 

 

Muhaji alisema wananchi wanapaswa kujua kuwa serikali inawekeza fedha nyingi ili wananchi na wenye viwanda wawe na uhakika wa umeme hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuvitunza.

 

“Tumewaleta wahariri kutembelea miradi ya Tanesco kwa sababu tunaamini mko karibu na wananchi na mtaawaambia umuhimu wa kutunza miundombinu ya umeme kwani hii ni kwa manufaa yaa Watanzania wote, wawekezaji na wafanyabiashara wadogo na wakubwa,” alisema.

 

 

“Vituo vya kupoza umeme viko karibu na wananchi na wako karibu sana na vituo vya umeme. Tunaamini hawa ndio walinzi wa kwanza wakiona mambo ambayo yanaonekana kutaka kuhujumu miundombinu watuambie mapema,” aliongeza.

 

 

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Mhandisi Herini Mhina, alisema kulikuwa na baadhi ya watu wanaojaribu kuhujumu miundombinu ya shirika hilo kwa kuiba nyaya lakini hivi sasa wamejitahidi kuimarisha ulinzi.

 

 

Alisema kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama wamefanikiwa kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafikisha kwenye mamlaka husika kwaajili ya hatua zaidi.

 

 

“Kuna watu walikuwa wanakata nyaya na ukiangalia wanavyokata si kwaajili ya kwenda kuuza ni kama hujuma kwasababu mtu anakata kakikapande kidogo ambako ukiangalia si kwamba anakwenda kuuza bali kuhujumu tu shirika,” alisema Mhina.

 

 

Habari Kubwa