Tani 1,000 za korosho zakataliwa kisa ubora

27Jan 2019
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe Jumapili
Tani 1,000 za korosho zakataliwa kisa ubora

TANI 1,000 za korosho kutoka kwa wakulima wa vyama vya msingi vya Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara, ambazo zimehifadhiwa kwenye ghala la Chama cha Ushirika cha Msingi (Amcos) cha Tuaminiane mjini hapa, zimekataliwa kupokewa kwenye ghala kuu la Buko kwa madai ya kukosa ubora.

Aidha,baadhi ya tani za korosho hizo zimehifadhiwa nje baada ya kukataliwa kupokelewa kwenye ghala hilo kuu kutokana na madai ya kukosa ubora hasa wa daraja la kwanza.

Hali hiyo, imesababisha baadhi ya tani kwenye chama hicho cha Tuaminiane kumwagwa chini nje ili zichaguliwe na zipangwe upya kwa madaraja stahiki.

Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Tuaminiane, Dismas Hamushila, alisema hadi sasa kwenye ghala lake kuna mrundikano mkubwa wa magunia ya korosho kati ya tani 500 na 1,000 ambazo zimekataliwa kuingia kwenye ghala kuu la Buko.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kukataliwa kwa korosho hizo kwenye ghala hilo ni kutokana na madai ya kukosa ubora na ili zipokewe, zinatakiwa kuchaguliwa upya.

Mwenyekiti huyo alisema korosho hizo ambazo zinadaiwa kukosa ubora, zinatoka katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji Masasi, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na Nanyumbu.

Kutokana na sakata hilo, alisema korosho hizo tangu zilipopokewa kwenye chama hicho, ni mwezi mmoja sasa na haijulikani lini zitatoka kwenda ghala kuu zikiwa tayari zimeshachaguliwa upya.

Hamushila alisema kutopokewa kwa korosho hizo kwenye ghala kuu, kumesababisha adha kubwa kwenye ghala lake ambalo limesheheni tani za korosho na kufanya baadhi ya tani kuhifadhiwa nje sakafuni zikisubiriwa kumwagwa chini kwa ajili ya kuchaguliwa upya.

“Serikali imetupa maagizo ya kwamba ifikapo Januari 30, korosho zote zilizoko kwenye mghala ya vyama vya msingi ziwe tayari zimeshakwenda maghala makuu lakini shida iliyopo hapa kwangu na kazi ya kumwaga chini na kuzichagua, naona kama agizo kwangu litakua gumu,” alisema Hamushila

Alisema ili kufanikisha kuchagua korosho, kunahitaji fedha nyingi kwa vyama vya msingi ili kuwalipa vibarua wanaofanya kazi ya kuchagua ambao wengi wao ni kinamama.

Pia alisema kazi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu baadhi ya vyama vya msingi kwa sasa havina fedha za kuwalipa vibarua hao, hivyo kusababisha mrundikano wa korosho zikiwa nje chini na zingine ndani.

Kutokana na mrundikano wa korosho kwenye ghala lake, anaiomba serikali kuangalia namna ya korosho hizo kupokewa katika ghala kuu kwa kuwa zipo za daraja la kwanza na lipi, hivyo kuzikataa zote ni kutowatendea haki wakulima.

Kuhusu malipo ya korosho kwenye chama chake, Hamushila alisema serikali imeshawalipa baadhi ya wakulima na kwamba wale ambao wao wana zaidi ya kilo 1,500 ni 205 na walifikiwa kwa ajili ya kuhakikiwa ni wanane pekee huku 198 wakiwa hawajahakikiwa.

Mmoja wa wakulima wa korosho ambaye ameuzia korosho zake kwenye ghala la Tuaminiane, Muhaji Saidi, alisema wanashangazwa kuona korosho zao zikikataliwa kupokewa kwenye ghala kuu kwa madai kuwa zimekosa ubora.

Saidi alisema katika misimu yote iliyopita korosho za aina hiyo zilikuwa zikipokewa bila kuwekwa mashariti ya aina yoyote hivyo kushangazwa tunashangzwa na utaratibu wa msimu huu kuelezwa kuwa wanapaswa kuzichagua ili ziwe kwenye ubora.

Ashura Adam, Mwenyekiti wa Nanyumbu Amcos, aliomba korosho zao zipokewe kwenye maghala makuu hata kwa kuwekwa kwenye daraja la pili kwa kuwa hawajui hatima ya korosho zao iwapo zitaendelea kukataliwa.

“Tumekwama sana kwa suala hili kwani korosho zetu tunaambiwa hazina ubora lakini bado tunaziona zina ubora. Tunaambiwa tuchague sasa ni lini tutamaliza kufanya kazi hii na kuingizwa kwenye ghala kuu,” alisema.

 

Mkuu wa Ghala Kuu la Buko, Aisha Ramadhani, alikiri kuwa baadhi ya tani za korosho zimekataliwa kuingia katika ghala hilo kwa sababu hazina ubora wa daraja la kwanza kwa kuwa katika ghala hilo korosho zilizomo ni za daraja la kwanza pekee.

Alisema licha ya korosho hizo kukosa ubora, ziko baadhi ni ndogo ndogo, hivyo kusababisha ubora unaotakiwa lakini sababu nyingine ni kwamba ghala hilo kwa sasa limesheheni korosho na hakuna sehemu iliyosalia ya kuhifadhi zingine hasa zilizo katika daraja la pili.

Akiwa katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Mbuyuni, Masasi hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, alisema wakulima waendelee kuwa na subira kuhusu malipo ya korosho na kwamba serikali bado inaendelea kuwalipa fedha zao kwa kufuata taratibu ikiwamo kuhakikiwa majina ili kujiridhisha kuwa mkulima anayelipwa ni sahihi .

Alisema kila mkulima ambaye serikali itajiridhisha kuwa korosho alizopeleka ghalani ni zake, lazima atalipwa haki yake, hivyo kwa sasa hakuna sababu ya kuilamu serikali kuwa inachelewesha malipo yao.

 

 

Habari Kubwa