Tani 30 za ruby zachimbwa Longido

08Dec 2021
Woinde Shizza
ARUSHA
Nipashe
Tani 30 za ruby zachimbwa Longido

ZAIDI ya tani 30.8 za madini aina ya ruby yenye thamani ya Sh. bilioni 3.165 zimechimbwa katika Mgodi wa Sendeu Agrovet Co. Ltd ulioko wilayani Longido mkoani Arusha.

Hayo yalibainishwa na mmiliki wa mgodi huo, Sendeu Laiza, alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya Waziri wa Madini, Doto Biteko, mgodini huko na kuona jinsi wanavyoendesha shughuli zao.

Alibainisha kuwa uchimbaju rasmi wa madini ya ruby katika Kijiji cha Mundarara ulianza mwaka 1948 na ukianza na kampuni ya kigeni iliyokuwa imesajiliwa Kenya ya Continental Ore Company Ltd.

Sendeu alisema baada ya Tanganyika kupata Uhuru mwaka 1961, serikali ilitaifisha mgodi huo mwaka 1973 na kukabidhiwa kwa Tanzania Gemstone Industries ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Alisema kuwa tangu kukabidhiwa kwa mgodi huo kwa kampuni yake mwaka 2009, zaidi ya tani 30.8 za madini ya ruby zimechibwa katika mgodi huo.

Akiwa mgodini huko, Waziri Biteko aliipongeza kampuni ya Sendeu Agrovet Co. Ltd kwa kupata madini hayo na kuwataka wachimbaji wa madini ya ruby kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana.

Waziri huyo alisema kuwa mahali popote penye ridhiki, hapakosi migogoro, hivyo alimwomba  Sendeu akae vizuri na watu ili kuepusha migogoro kwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona wachimbaji wanatajirika.

Alisema serikali itaendelea kumuunga mkono mmiliki wa leseni ya uchimbaji wa ruby, Sendeu Laiza na kumtaka achimbe kwa kufuata sheria na kuzingatia kulipa kodi za serikali.

Waziri Biteko alibainisha kuwa uwapo wa madini ya rudy katika Kijiji cha Mundarara ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wa Mundarara Wilaya ya Longido na kwa Watanzania wote.

Alitoa wito kwa wachimbaji, wafanyabiashara wa madini na wadau wote kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuongeza tija na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na stahiki ya serikali.

Habari Kubwa