Tani 8,000 za korosho kuingizwa mnadani Mtwara

14Oct 2021
Abdallah Khamis
MTWARA
Nipashe
Tani 8,000 za korosho kuingizwa mnadani Mtwara

JUMLA ya tani 8,292 za korosho zinatarajiwa kuingizwa sokoni katika mnada wa korosho utakaofanyika kesho mkoani Mtwara kwa kuvihusisha  vyama vikuu viwili vya Ushirika vya Tandahimba na Newala (TANECU),pamoja na kile cha Mtwara na Masasi (MAMCU).

Kiwango hicho cha korosho zinazotarajiwa kuingizwa mnadani kesho kwa kuvishirikisha vyama hivyo  vikuu  viwili vya ushirika  ni mara tano zaidi ya tani zilizouzwa siku ya kwanza ya ufunguzi wa msimu wa uuzaji  wa zao hilo, kwenye mnada uliowahusisha TANECU peke yao ambapo jumla ya kampuni 16 zilijitokeza kuomba kununua kwa bei tofauti tofauti.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti, Kaimu Meneja wa MAMCU Biadia Mpika na Mwenyekiti wa TANECU, Mohamed Nasoro, wamesema maandalizi yote ya mnada yamekamilika.

Mpika, amesema kwa upande wa MAMCU wanatarajia kuingiza mnadani tani 5,098,879, huku mwenyekiti wa TANECU akieleza kuwa wanatarajia kuingiza sokoni tani 3,194

"Sisi MAMCU huu ndiyo utakuwa mnada wetu wa kwanza kwa msimu huu tokea ufunguzi rasmi ulipofanyika wiki iliyopita,tutaingiza tani zaidi ya 5,000 maandalizi yote yamekamilika na tunaamini wakulima watapata bei nzuri kutoka kwa wanunuzi"amesema Mpika.

Ameeleza kuwa kwa MAMCU mnada utafanyika katika eneo la Mrina katika wilaya ya Masasi kuanzia saa 2 asubuhi.

Mwenyekiti wa TANECU,Mohamed amesema kwa upande wao mnada huo utakuwa ni wa pili baada ya msimu kufunguliwa na kwamba wataingiza sokoni tani 3,194.

"Kama ambavyo tulianza vizuri katika mnada wa kwanza wiki iliyopita na kesho tutafanya vizuri zaidi kwani tutaingiza tani nyingi tofauti na zile za mwanzo na kila kitu kimeshaenda sawa,tupo kwa ajili ya kusimamia maslahi ya wakulima na imani yetu watanufaika kupitia korosho"amesema Mohamed.

Mohamed ameeleza kuwa TANECU watafanyia mnada wao wa pili katika wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara na kuwahiza wakulima kuhudhuria kwa wakati kwa ajili ya kushuhudia mnada huo.

Habari Kubwa