Tanroads yatoa angalizo wizi miradi barabara

20Jul 2019
Joctan Ngelly
KIGOMA
Nipashe
Tanroads yatoa angalizo wizi miradi barabara

WAKALA wa Barabara Tanzania (Tanroads) umewapa angalizo wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuacha tabia ya wizi wa kutumia silaha kwenye miradi ya ujenzi wa barabara za lami.

Angalizo hilo lilitolewa na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mfungale, jana kwenye ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami katika Kijiji cha Kabingo hadi Kibondo, Kasulu, Buhingwe na Manyovu.

Alisema Barabara hii ya Kabingo, Kasulu, Manyovu na Rumunge hadi Oitaza upande wa Burundi ni sehemu ya mtandao wa barabara za Afrika Mashariki, na ndiyo maana mwakilishi kutoka Burundi alikuwapo kwa ajili ya mradi huo ambao utazinufaisha pia nchi za Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC).

Barabara za Kabingo na Kasulu ni kiunganishi cha mtandao wa barabara kwa upande wa magharibi mwa Tanzania.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Afrika ambayo imeshatoa jumla ya Sh. bilioni 500 na serikali ya Tanzania itachangia Sh. bilioni 58 ya mradi huo kwa mujibu mkataba uliotiwa saini kati yao na Benki ya Afrika.

Mhandisi Mfugale alibainisha kuwa kuna wizi mdogo mdogo kwenye miradi ambapo baadhi ya watu wanaiba mafuta, nondo na mabati, ingawa alisema ni jukumu la mkandarasi kudhibiti vitendo hivyo.

Mhandishi Mfugale alieleza zaidi jkuwa ana imani na wananchi wa Mkoa wa Kigoma, kwamba watatoa ushirikiano kuhakikisha vitendo hivyo vya wizi havitokei.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mfugale alisema kuna maeneo wananchi wanataka wakati wameshalipwa kwa muibu wa sheria, hivyo kusababisha miradi ya barabara kuchelewa kuanza.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi mradi huo, alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika itatoa Sh.trilioni moja, na kuishukuru kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi yake ya kuimarisha barabara za lami.

Ndalichako alisema changamoto zilizopo katika sekta ya barabara ni nyingi zikiwamo zile za uhamishaji wa miundombinu ya maji, hivyo kuomba kuwahakikishia wadau wa barabara serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Kigoma watafanya kila la ziada kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa ndani ya muda mfupi.

Habari Kubwa