"Tanzania tunayo Taasisi ya kutengeneza chanjo magonjwa ya mlipuko"

12Jun 2019
Zanura Mollel
Longido
Nipashe
"Tanzania tunayo Taasisi ya kutengeneza chanjo magonjwa ya mlipuko"

Naibu Waziri wa Mifugo Abdallah  Ulega amesema kwa sasa Tanzania inauwezo wa kutengeneza chanjo ya kudhibiti baadhi ya magonjwa ya mlipuko katika Taasisi ya TVI  iliyopo Kibaha ikiwemo dawa ya ugonjwa wa Kimeta ambayo imekuwa tishio kwa mifugo,wanyamapori na binadamu.

Naibu Waziri Wa Mifugo Abdallah Ulega akikagua maabara ya majaribio mpaka Wa Namanga juu yanudhibiti Wa homa ya bonde la ufa.

Amesema hayo kwenye ufunguzi wa zoezi la majaribio ya udhibiti wa magonjwa ya mlipuko  hususani homa ya bonde la ufa ( Rift valley fever) utakaoendeshwa kwa siku nne katika eneo la mpaka wa Namanga unaoinganisha nchi ya Tanzania na Kenya.

Ameeleza kuwa, wizara yake imejipanga vizuri dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa mifugo, na zoezi hilo linaloendelea lipo chini ya Umoja wa Afrika Mashariki. 

Amefafanua kuwa, kuna wataalamu wakutosha wanaoshughulikia magonjwa haya pindi yatokeapo."Mifugo ya Tanzania ni salama kwani wanapatiwa chanjo mara kwa mara,lakini pia tuna wataalamu wetu katika vituo hivi vya pamoja (OSBP) na katika maeneo  mikoani," Amesema Ulega 

Amedai kuwa mifugo mingi ya Tanzania inauzwa nchi jirani ya Kenya, nakuwataka wananchi jirani wa kenya kuondoa hofu juu ya mifugo hiyo, kwani kabla haijapelekwa huko kibiashara inafanyiwa ukaguzi na vipimo mbali mbali na wataalam na endapo ikabainika kuwa na ugonjwa hawezi kusafirishwa kibiashara kwenda nchi nyingine.

"Magonjwa haya yanatoka kwa mifugo kwenda kwa wanyamapori hadi kwa binadamu hususani kimeta,tumejipanga ipasavyo,tunayo taasisi inayojihusisha na utengenezaji wa chanjo ya kimeta ikiwemo taasisi ya TVI iliyopo kibaha" amesema Ulega

Bahati Saitoti mkazi Wa Namanga Tanzania alisema kuwa miezi michache iliyopita ugonjwa Wa kimeta ulivyamia katika eneo la Wilaya ya Longido, lakini alishuhudia chanjo zikitolewa kwa wakati muhafaka,na kuiomba serikali kuongeza watumishi Wa kutosha katika idara ya Mifugo 

" Wilaya ya longido ni Wilaya ya kifugaji,tunaomba serikali iongeze nguvu kazi kwa kuhakikisha dawa zinapatikana pamoja na wataalamu wakutosha ili yanapotokea magonjwa ya mlipuko waweze kutoa huduma kwa wakati" alidai Saitoti

Mkurugenzi Huduma ya Afya na Mifugo, Dk. Herzon Nonga, amesema ugonjwa wa homa ya bonde la ufa uligundulika nchini Tanzania mwaka 1930 na ugonjwa huu unatabia ya kujitokeza kila baada ya miaka 7 hadi 10 na kwa hapa nchini imeshawahi kuripotiwa kutokea kwa miaka 10.

" Ugonjwa huu chanzo chake ni Virusi viitwavyo Phlebovirus na huishi kwenye mayai ya mbu aitwaye Aedes,lakini pia huishi kwenye vumbi kwa muda mrefu na kuanguliwa wakati Wa mvua ( Mafuriko)" amedai Dk. Kongo

Hata hivyo amegusia kuwepo kwa ugonjwa huo katika nchi ya Tanzania na Kenya kwa miaka  ya 2006/2007 na kuleta athari ya zaidi ya shilling I billion 149 kutokana na Wizara husika juu ya udhibiti wa magonjwa hata kutokuwa na utayari na maandalizi ya kukabiliana na magonjwa hayo.

" Ugonjwa huu uliua sana Mifugo ,wanyamapori na binadamu hivyo baraza la mawaziri la afrika mashariki march 24/ 2015 liliweka azimio kwa kila nchi wanachama kuweka mikakati juu ya kukabiliana na magonjwa yalipuko katika maeneo yao hususani mipakani" alisema Dr Kongo

Hata hivyo alifafanua kuwa ,ukanda Wa afrika mashariki umekuwa na matukio mengi ya magonjwa yanayoambukizwa kwa binadamu kupitia wanyama ,na hii ni kutokana na uwepo Wa wanyama wengi,Mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na mazingira rafiki kwa vimelea vya magonjwa

Habari Kubwa