Tanzania, China zaahidi kuendeleza ushirikiano

11Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Tanzania, China zaahidi kuendeleza ushirikiano

TANZANIA na China zimeahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia ili kuhakikisha pande zote zinakuwa na maendeleo endelevu.

Makubaliano hayo yalifanywa na Balozi wa China nchini, Wang Ke, wakati alipokutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, jana jijini Dar es Salaam.

Balozi Ibuge alisema wamejadiliana masuala mbalimbali ikiwamo namna ya kutekeleza nia ya viongozi wakuu wa Tanzania, Rais John Magufuli na Rais wa China, Xi Jinping, ya kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa wa COVID19 ikiwamo kufutiwa na kusamehewa madeni.

“Naishukuru serikali ya China kwa uhusiano na ushirikiano ambao imekuwa ikionyesha kwa Tanzania. Uhusiano huo umeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku na serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wa kidiplomasia kati yake na China.

Pamoja na mambo mengine, mazungumzo yalihusu masuala ya biashara na uwekezaji, mradi wa nyumba 25 za wataalum wa afya zilizoko Osterbay, jijini Dar es Salaam.

Balozi Wang Ke, pamoja na mambo mengine, aliipongeza serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizochukua katika kukuza uchumi wake hadi kufikia uchumi wa kati pamoja na mapambano dhidi ugonjwa wa corona.

"Leo (jana) nimekutana na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje, Balozi Ibuge na kuzungumza mambo mbalimbali ya ushirikiano.

Tunaipongeza serikali ya Tanzania kwa jitihada ilizochukua katika kufanya kazi kwa bidii na kukuza uchumi wake hadi kufikia uchumi wa kati pamoja na hatua ilizochukua katika kupambana na janga la COVID 19 ambapo tumefurahishwa kuona janga hili limeisha," alisema Balozi Ke.

Balozi Ke aliongeza kuwa wamekubaliana katika mazungumzo hayo pia kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya pande zote ili kuhakikisha uhusiano na ushirikiano unazidi kukua na kuimarika.

Tanzania na China zimekuwa zikishirikiana katika sekta za kilimo, biashara na uwekezaji, miradi ya mikopo nafuu na misaada, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), uchukuzi, afya, utalii na utamaduni.

China na Tanzania zilianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1964.

Habari Kubwa