TANZANIA imetajwa kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na simba wengi barani

08Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
TANZANIA imetajwa kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na simba wengi barani

TANZANIA imetajwa kuwa nchi inayoongoza kwa kuwa na simba wengi barani Afrika.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa African Wildlife Foundation, Kaddu Sebunya, wakati akizungumza kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na mazingira kwa nchi za Afrika.

Sebunya alisema kwa upande wa tembo, Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na tembo wengi.

“Hii inatokana na juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha wanyamapori na uhifadhi wa misitu unapewa kipaumbele,” alisema.

Alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa nchi zingine katika suala la uhifadhi wa misitu na utunzaji wa wanyamapori.

Sebunya aliitaja nchi ya kwanza inayoongoza kwa kuwa na tembo wengi kuwa ni Botswana ikifuatiwa na Zimbabwe.

“Kuna umuhimu wa kila nchi ya Afrika kuweka mikakati itakayosaidia maliasili zake zitunzwe na kulindwa ipasavyo,” alisema.

Aidha, alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni upungufu wa wanyamapori hasa simba na tembo kwa sababu ya kuwapo kwa majangili na uwindaji haramu.

Kutokana na hali hiyo, Sebunya alisema African Wildlife Foundation, inahamasisha kila nchi kuweka mipango ambayo itasaidia kuwafanya simba na tembo waendelee kuwapo.

Alisema endapo kila nchi ikiamua kulinda wanyamapori na uhifadhi hakuna ambacho kitashindikana.

“Mfano mzuri ni Tanzania miaka ya nyuma tembo walikuwa wanauawa, lakini kwa sasa wako salama kutokana na hatua ambazo serikali imezichukua,” alisema.

Habari Kubwa