Tanzania kuhudhuria Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama

10Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Tanzania kuhudhuria Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama

​​​​​​​TANZANIA inatarajiwa kushiriki Mkutano wa 26 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika kuanzia Novemba mosi hadi 12, 2021 mjini Glasgow nchini Uingereza.

Hayo yamebainika leo Juni 10, 2021 wakati wa kikao kati ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar kilichofanyika ofisini kwa Waziri Jafo jijini Dodoma leo Juni 10, 2021.

Waziri Jafo amesema kuwa mkutano huo utakaofanyika utatoa mchango mkubwa katika sekta ya mazingira kwani nchi mbalimbali zitakutana na kujadili namna gani ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kupunguza hewa ya ukaa duniani na ukataji wa miti.

Pia, Waziri huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kukuza uhusiano wa kidiplomasia na nchi mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoa mchango katika hifadhi ya mazingira.

“Changamoto ya mazingira imekuwa ni kubwa kwa hiyo ni jukumu letu Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Sera na kuratibu shughuli zote za mazingira na kuhakikisha nchi yetu inakuwa kinara katika uhifadhi mazingira,” amesema Jafo.

Pia aliwaomba wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuungana kwa pamoja na kuifanya Tanzania kuwa ya mfano katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanayoikabali nchi yetu.

Habari Kubwa