Mkutano huo unawakutanisha watunga sera na wafanya uamuzi katika ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali duniani. Pamoja na mambo mengine, watajadili masuala ya kisera katika kuendeleza uwindaji.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Maliasili na Utalii ilieleza kuwa Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Damas Ndumbaro, anatarajia kunadi fursa za uwekezaji za uwindaji wa kitalii kwa lengo la kuwawezesha matajiri wakubwa duniani kuchangamkia uwekezaji huo nchini.
“Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amewasili jijini New York, Marekani, anatarajia kunadi fursa za uwekezaji za uwindaji wa kitalii zilizoko nchini kwa lengo la kuwawezesha matajiri wakubwa duniani kuchangamkia uwekezaji huo uliopo hapa nchini,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema Tanzania ni mshiriki muhimu katika mkutano huo kwa sababu ni moja ya nchi zinazoongoza duniani katika uhifadhi wa wanyamapori na uwindaji.
Pia taarifa hiyo ilisema kupitia mkutano huo itaweza kuongeza uelewa zaidi katika masuala ya kisera na uamuzi katika kuendeleza sekta ya uwindaji wa kitalii nchini.
Dk. Ndumbaro, kwa mujibu wa taarifa hiyo, atapata fursa ya kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa masuala ya utalii ikiwa sehemu ya kuwavutia kuja nchini kuwekeza.
“Katika mkutano huo, Waziri Ndumbaro ameambatana na Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dk. Maurus Msuha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali Hamis Semfuko na Kaimu Kamishna Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi.
“Wengine ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Lulu Ng'wanakilala na Ofisa Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori wa kutoka TAWA, Segolin Tarimo.” Ilibainisha taarifa hiyo.
Waziri Ndumbaro pamoja na ujumbe wake wamepokewa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Elsie Kanza.