Tanzania yajipanga kuuza umeme nje

28Feb 2021
Joseph Mwendapole
Morogoro
Nipashe Jumapili
Tanzania yajipanga kuuza umeme nje

SERIKALI imetangaza kuwa bei ya umeme itashuka na itakuwa na akiba ya kuziuzia nishati hiyo nchi jirani baada ya kukamilika kwa bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere Juni mwakani.

Hayo yalibainishwa jana mkoani Morogoro na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alipofungua mkutano wa siku mbili wa wahariri na waandishi wandamizi.

Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Shirika la Umeme (TANESCO) kwa ajili ya kutembelea bwawa hilo litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,150.

Waziri Kalemani alisema bei ya umeme itashuka kwa sababu uzalishaji wa nishati hiyo kwa njia ya maji ni rahisi kulinganisha na uzalishaji kwa njia zingine kama mafuta.

Alitoa mfano uzalishaji wa uniti moja ya umeme kwa njia ya maji ni Sh. 30 hivyo kuna neema ya gharama ndogo ya umeme kwa Watanzania mara tu mradi huo utakapokamilika.

Alisema mpaka kufikia mwaka 2023, Tanzania kupitia vyanzo vyake mbalimbali vya kuzalisha umeme, itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 4,881 wakati mahitaji hayatazidi megawati 2,700 kwa wakati huo.

Alisema nchi itakuwa na akiba ya megawati 2,100 ambazo zinaweza kuuzwa kwa nchi jirani zenye uhaba wa nishati hiyo.

Waziri Kalemani alipongeza uamuzi wa Rais John Magufuli kujenga bwawa hilo ambalo litaihakikishia nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika, hivyo kuwavutia wawekezaji wengi kuwekeza nchini.

Alisema ujenzi wa bwawa hilo haujasababisha na wala hautasababisha uharibifu wowote wa mazingira kwa kuwa sehemu iliyotumika ni ndogo kulinganisha na ukubwa wa eneo la Selous.

"Badala yake uzalishaji wa umeme kwenye bwawa hili utapunguza uharibifu wa mazingira kwa sababu ukataji miti kwa ajili ya mkaa utapungua sana, hivyo tunapaswa kujivunia ujenzi wa mradi huu," alisema.

Alisema imekuwa kawaida kuona maelfu ya magunia ya mkaa yakiingia mkoani Dar es Salaam kutokana na ukataji wa miti, jambo ambalo litapungua iwapo kutakuwa na umeme mwingi wa kutosha.

"Ukipiga hesabu ya magunia ya mkaa yanayotumika kwa mwaka mmoja tu, utaona namna gani mazingira yetu yanavyoharibiwa sasa, ukipiga kwa miaka 10 athari zake ni mbaya sana.

"Ndiyo maana Watanzania tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Magufuli kwa ujasiri wake wa kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa sababu faida zake ni nyingi sana kwa uchumi wetu," alisema.

Habari Kubwa