Tanzania yapaa mapambano ya rushwa

11Feb 2019
Salome Kitomari
Addis Ababa, Ethiopia
Nipashe
Tanzania yapaa mapambano ya rushwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema nchi za Bara la Afrika zimeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa.

Waziri Mkuu, akipata kando ya picha mbalimbali za viongozi wa Afrika waliopigania uhuru,anayoitazama ni ya Mwalimu Julius Nyerere,picha hizo zimebandikwa kwenye korido za ukumbi wa mikutano wa AU,Addis Ababa,Ethiopia.

 

Ameyasema hayo leo Jumatatu, Februari 11, 2019 wakati akitoa muhtasari wa yaliyojiri kwenye Mkutano wa 32 wa Wakuu wa nchi za Afrika (AU) unaofanyika Addis Ababa, Ethiopa.  

Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mkutano huo amesema katika mkutano huo pamoja na mambo mengine Serikali barani Afrika zimesisitizwa kupambana na wala rushwa, ambapo Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika mapambano hayo. 

Mbali na kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa, pia Waziri Mkuu amesema ripoti ya kamati maalumu iliyoundwa kuhusu masuala ya afya inaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri. 

Waziri Mkuu amesema Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia na kudhibiti malaria, mapambano dhidi ya ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi mpaka vijijini.

Habari Kubwa