Tanzania yapiga hatua ubora huduma ya choo

20Nov 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Tanzania yapiga hatua ubora huduma ya choo

WIZARA ya Afya imesema kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita vyoo bora katika ngazi ya kaya vimeongezeka kutoka asilimia 19.5 kwa mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 72.6 mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe.

Pia imesema kaya zisizokuwa na vyoo kabisa zimepungua kutoka asilimia 20.5 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 1.4 mwaka huu, huku ikibainisha mtu mmoja ambaye hana choo hupoteza takriban saa 58 kwa mwaka kutafuta mahali pa kujisitiri.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe alibainisha hayo jana jijini hapa kwenye kilele cha wiki ya usafi na maadhimisho ya siku ya matumizi ya choo duniani.

Pia alisema ujenzi wa vyoo bora pamoja na kuwapo huduma za maji safi na salama umeongezeka katika taasisi zikiwamo shule za msingi na vituo vya kutolea huduma za afya.

"Ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita takriban shule za msingi 2,500 zimejengewa vyoo bora, vituo vya kutolea huduma za afya vipatavyo 1,500 vimeboreshewa huduma ya maji, vyoo na sehemu za kunawa mikono," alisema.

Alibainisha kuwa ufuatiliaji uliofanywa na wizara hiyo kwa mwaka huu unaonyesha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, zaidi ya vituo vya njiani 280 vyenye vyoo bora vimejengwa na serikali na sekta binafsi, hali iliyopunguza abiria kujisaidia ovyo safarini.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya, Mazingira wa Wizara ya Afya, Anyitike Mwakitalima alisema mtu mmoja ambaye hana choo hupoteza takriban saa 58 kwa mwaka kutafuta mahali pa kujisitiri, akifafanua ni muda mwingi kwa nchi inayotaka kupiga hatua kiuchumi.

Alisema kuwapo huduma ya maji, vyoo bora na sehemu za kunawa mikono kumethibitika kuchangia kupungua kwa vifo vya kinamama wakati wa kujifungua kwa kati ya asilimia 17 hadi 25.

"Imethibitika kwamba ukosefu wa huduma hizi husababisha hadi asilimia 45 ya vifo vya watoto wachanga," alisema.

Mwakitalima alisema shule zenye huduma bora za maji na vyoo zimethibitika kuwa na mahudhurio mazuri kwa watoto wote kulinganishwa na zenye huduma duni.

Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh. bilioni 104 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usafi na huduma za maji kwenye shule na vituo vya afya.

"Kiasi hiki kinatumika kwenye shule za msingi 1,500 na zaidi ya vituo vya huduma za afya 2,500. Aidha, serikali imeandaa fedha kupitia mradi wa BOOST chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia ambao utawezesha ujenzi wa miundombinu bora ya usafi kwa shule zaidi ya 6,000 ifikapo mwaka 2025," alisema.

Mwaka 2025 ni ukomo wa upimaji wa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014. Pia ni ukomo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Junin 1999-2025 inayolenga kupunguza walau nusu ya wananchi wanaoishi katika umaskini na kuwafanya waishi katika uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Habari Kubwa