Tanzania yapigwa jeki ujenzi wa reli ya kisasa

14Feb 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Tanzania yapigwa jeki ujenzi wa reli ya kisasa

BENKI ya Standard Chartered imesaini makubaliano ya kuikopesha Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango Dola za Marekani bilioni 1.46 (sawa na Sh. trilioni 3.3), kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya pili wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini, Sanjay Rughani, wakibadilishana makabrasha, jijini Dar es Salaam jana, baada ya kusaini makubaliano ya mkopo wa Sh. trilioni 3.3 kwa Serikali ya Tanzania. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kipande hicho kina urefu wa kilomita 550 katika mkakati wa kuboresha njia za usafiri nchini.

Akizungumza jana wakati wa kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo nchini, Sanjay Rughani, alisema kwa miaka 103 ya uwepo wa benki hiyo nchini mkataba huo ni wa kihistoria kuwahi kufanyika baina yake na serikali.

Alisema utasaidia kupunguza tatizo la usafiri na usafirishaji wa mizigo pamoja na kuokoa muda unaopotea katika shughuli za usafiri kwa treni za kawaida ambazo haziendi kasi kama ilivyo kwa treni za kisasa.

“Mkataba huu utaenda kugusa maisha ya watu wengi na hakuna kitu kizuri katika maisha kama kusaidia wengine,” alisema Rughani.

Akizungumza kuhusu mkopo huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kufika mpakani mwa Uganda, Rwanda, Burundi na Kigoma kukamilika kwa wakati na kusaidia kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi, kukuza kilimo na kuboreshwa kwa huduma za kijamii.

“Mkopo huu ni takribani Sh. trilioni 3.3 za wale wanaosema kuwa deni la taifa linakuwa niendelee kusisitiza kuwa deni la taifa ni himilivu,” alisema Dk. Mpango.

Kwa mujibu wa waziri huyo, ni muhimu kukopa kwa kuwa uwekezaji huo ni wa hadi miaka 200 ijayo na kwamba reli hiyo itaenda kwa kasi na kubeba mzigo mkubwa kuliko iliyopo sasa, kukuza uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja, kukuza kilimo na biashara.

“Kuna baadhi ya wabia wetu tena wa siku nyingi tu tuliwaomba waingie kwenye safari hii kwenye kuchangia hili na ni mkopo wala siyo kwamba wanatupa bure, lakini wametukatalia kwa hiyo Standard Chartered hawa tunawashukuru sana,” alisema Dk. Mpango.

Habari Kubwa