Tanzania yapongezwa kuzuia mifuko ya plastiki

17May 2019
Na Mwandishi Wetu
GENEVA
Nipashe
Tanzania yapongezwa kuzuia mifuko ya plastiki

SHIRIKA la Kimataifa la kutetea na kulinda Wanyama, limeipongeza Tanzania kwa kuzuia matumizi ya plastiki, kwa kuwa ni uamuzi mkubwa wa kulinda mazingira kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na majanga duniani, Scott Cantin.

Akizungumza na Nipashe mjini Geneva, nchini Switzerland, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na majanga duniani, Scott Cantin, alisema uchafuzi wa mazingira ya bahari usipochukuliwa hatua madhubuti ni janga jingine kwa dunia.

Alisema uamuzi wa serikali kuwa na sheria na sera zinazolinda mazingira hasa kwenye eneo la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ni wa kupongezwa na unastahili kuungwa mkono.

Alisema shirika hilo pia linafanya kampeni ya kulinda uchafuzi wa bahari kwa kutumia plastiki, kwa kushirikiana na jamii za maeneo husika kusafisha fukwe za bahari.

“Plastiki ni hatari kwa mazingira na bahari kwa ujumla kwa kuwa yanaweza kuua viumbe hai ikiwamo samaki, lakini zinaweza kuishi kwenye mwili wake na kuliwa na binadamu kisha kuleta madhara makubwa kwa afya zao,” alisema.

 

Alisema kwa nchi zinazopiga marufuku matumizi ya plastiki zinastahili kuigwa kuwa wamebaini chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.

“Tunafahamu kuwa plastiki zinaishi kwenye ardhi kwa zaidi ya miaka 500 kama hazijaondolewa na kuharibiwa,” alisema.

“Uamuzi wa Tanzania ni mzuri sana kwa kuwa sasa wanakwenda kupunguza kiwango cha plastiki zinazokwenda kwenye ardhi, vyanzo vya maji na habari. Hivi ndivyo nchi zinapaswa kufanya kwa kuwa na mpango endelevu wa kutunza mazingira kwa miaka mingi ijayo,” alisema.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu ya Umoja wa Mataifa, inakadiriwa kuwa miaka mitano hadi kumi ijayo kutakuwa na plastiki nyingi kwenye bahari, ambazo kwa kawaida zinaishi kwa zaidi ya miaka 500.

Aprili mwaka huu, serikali alitangaza uamuzi wa kupiga marufuku uzalishaji plastiki ifikapo Mei 31, na itakapofika Juni mosi, hakuna kuzalisha mifuko au kutumia plastiki ambazo hazina ubora unaotakiwa.

Februari mwaka huu, katika mdahalo ulioitishwa na Ubalozi wa Ufaransa nchini, mtafiti wa Mazingira na Afya wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, Hussein Mohamed, alisema upo uwezekano mkubwa wa plastiki kuwa chanzo cha maradhi ya saratani, mfumo wa uzazi na ini.

 

Mhandisi wa Viwanda Idara ya Mazingira ya Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Julius Mushi, alisema plastiki ni changamoto ya dunia kutokana na ukweli hudumu kwenye mazingira kwa miaka 500 hadi 1,000.

“Uchafuzi ukiendelea hivi utaathiri mazingira na afya zetu, lakini pia suala la kiuchumi. Taka zinapoingia kwa wingi kwenye bahari zitaathiri afya kupitia samaki, pia mifugo hupenda kula plastiki kutokana na chumvi chumvi iliyopo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mushi, takwimu zinaonyesha Tanzania inatumia mifuko bilioni mbili hadi tano, ikiwa ni wastani wa kila Mtanzania wa Bara kutumia mfuko mmoja hadi miwili kwa wiki.

“Kwenye uzalishaji tunazalisha tani 60,000 kwa mwaka za taka za plastiki na asilimia 70 hadi 80 huingia kwenye mazingira na hivyo kuathiri kwa kiwango kikubwa mazingira na maeneo ya ikolojia,” alifafanua.

Aidha, alisema Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, walifanya utafiti katika Ziwa Victoria kuangalia athari za plastiki kwenye samaki, walichukua samaki 40 kati yake asilimia 20 walikutwa na chembechembe za plastiki.

Habari Kubwa