Tanzania yasitisha shughuli mpaka Namanga

04Jun 2020
Daniel Sabuni
Namanga
Nipashe
Tanzania yasitisha shughuli mpaka Namanga

MPAKA wa Namanga upande wa Tanzania umesitisha shughuli zote za kibiashara na nchi jirani ya Kenya kwa muda kutokana na nchi hiyo kutoamini vyeti vya ugonjwa wa Covid -19 unaosababishwa na virusi vya corona vya madereva wa malori wa Tanzania vinavyoonyesha kuwa hawajaambukizwa.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe, ameiambia Nipashe jana kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya upande wa Kenya kukiuka makubaliano ya pande hizo mbili, waliyotiliana saini Mei, mwaka huu kwa kuzuia madereva wa Tanzania, kukataa vyeti ili wawaruhusu kuingia Kenya.

“Nadhani wenzetu wana ajenda ya siri kutuhujumu kiuchumi, tumeshakubaliana dereva anapopimwa upande wa Tanzania aruhusiwe upande wa Kenya kwa cheti, sasa wamekiuka makubaliano, wakifika upande ule wanataka wawapime tena sijui wana maana ipi nashindwa kuwaelewa kabisa, tumeamua kuchukua hatua na haturudi nyuma,” alisema.

Katika makubaliano hayo waliamua katika lori itaruhusiwa dereva na wasaidizi wawili kuingia katika nchi husika wote wakiwa wamepimwa kama wana maambukizo ya corona.

Hata hivyo, alisema upande wa Kenya wamebadilika juzi (Jumatatu) kwa kuzuia na kutaka kuwapima tena.

“Pamoja na juhudi za mimi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, kuwasiliana na viongozi wenzetu wa Kenya, lakini zimegonga mwamba na ndipo tukaamua kuzuia vyeti vyote na magari ya mizigo kutoka Kenya pamoja bidhaa zote zinazoingia kutoka nchini humo hadi hapo tutakapokaa tena na kufikia muafaka maana sote tunategemeana, Kenya wanatuhitaji kama soko na sisi wanatuhitaji pia ili kuuza bidhaa,” alisema Mwaisumbe.

Alisema mwezi Mei makubaliano ya kuruhusu kuaminiana pande mbili yalikaliwa kikao na mawaziri wa mambo ya nje za nchi, makatibu wakuu, wataalamu na viongozi wengine wa mikoa na wilaya wa kutoka nchi mbili katika mpaka wa Namanga, kufuatia mazungumzo ya Rais John Magufuli na Rais Uhuru Kenyata ambao waliwaagiza viongozi wanaohusika kukaa na kufanya vikao na makubaliano, huku wakichukua tahadhari za ugonjwa huo na kuona namna ya kuendelea na biashara kwa nchi hizo.

Alisema kama hali ya kutoaminiana itaendelea, itawalazimu kutoa uamuzi wa kuigeuza Namanga kuwa bandari kavu na majirani Wakenya watashusha mizigo au bidhaa upande wake na Tanzania kuichukua na pia hata Tanzania itapeleka wa Tanzania ili Kenya waifuate.

“Nchi yetu ni huru inayojitegemea haihitaji kubembeleza nchi nyingine kufanya biashara kwa sababu sisi tunategemeana, haiwezekani mambo ambayo yameagizwa na marais viongozi wa chini hawatekelezi…linaashiria dharau na ajenda ambayo wanadhani ni siri iliyofichika kumbe sisi tunaifahamu, hatutaweza kuivumilia hata kidogo,” alisema.

Alisema, nia ya Rais Magufuli ni kuwasaidia watu wa hali ya chini kwa kuwa uamuzi huo unapofanyika wanao umia ni watu wa chini.

“Nataka nikuhakikishie ndugu kupima kipimo cha Covid-19 sio lelemama kinaumiza sana, sasa haiwezekani siku mbili mtu amechokonolewa pua, halafu anatoka upande wa Tanzania anaenda upande wa Kenya anafanyiwa kitu kile kile, sasa hali hii kwa kweli sio sahihi, tunataka hiyo agenda yao ya siri ijitokeze hadharani tushughulike nayo kuliko kutumia ugonjwa wa Covid-19, sisi hatutakuwa tayari,” alisema Mwaisumbe.

Habari Kubwa