Tanzania yataka uhuru wa kisera

17Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tanzania yataka uhuru wa kisera

Serikali ya Tanzania imetaka kuwepo na uhuru wa kisera kwa nchi zinazoendelea na maskini ili kujihami na athari za uingizwaji uliokithiri wa bidhaa za kilimo hususan kutoka nchi zilizoendelea.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof.Kitila Mkumbo amesema hayo  katika Mkutano wa Mawaziri wa  Kundi la Nchi 33 (G33) wa wanachama wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) uliofanyika kwa njia ya mtandao ambapo aliongoza ujumbe kutoka Tanzania.

Kundi hilo linajumuisha nchi wanachama zenye maslahi yanayofanana ya kutaka uwazi na manufaa katika majadiliano ya WTO yanayohusu Kilimo ambapo lengo la mkutano ni kujadili na kuweka msimamo wa pamoja katika maeneo ya kipaumbele kwenye kilimo.

Katika mchango wake, Prof. Mkumbo amebainisha msimamo wa Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ambao unaungwa mkono na nchi nyingine wanachama kwenye eneo la misaada ya upendeleo (Domestic Support).

“Msimamo wa Tanzania ni kuwa na makubaliano ya WTO yanayokataza na kuweka vikwazo kwa nchi zilizoendelea wanachama wa Shirika hilo kutoa misaada kwa wazalishaji wao inayoathiri biashara za nchi nyingine wanachama. Hii ni pamoja na kutaka uwepo uwazi kwa  nchi ziluzoendelea kwa mfano katika utoaji ruzuku kwa wakulima wao,”amesema.