Tanzania yaweka mikoa 20 kimkakati kilimo korosho

23Nov 2020
Ashton Balaigwa
Singida
Nipashe
Tanzania yaweka mikoa 20 kimkakati kilimo korosho

TANZANIA imeweka mkakati wa kuliteka soko la korosho duniani kwa kuanza kupanua kilimo hicho kutoka mikoa mitano inayolima sasa hadi 20 kutokana na kuwapo kwa mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo.

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imeanza kuwanoa wakulima wa mikoa mbalimbali wakiwamo wa Singida kupitia zao hilo, linaloonekana kuwa bora kama ilivyo kwa mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara.

Kutokana na mkakati huo TARI kupitia kituo chake cha Naliendele mkoani Mtwara, kimezalisha aina 54 za mbegu bora za korosho za teknolojia ya kisasa na kuwapatia wakulima wa Wilaya ya Manyoni ambao wameanza kilimo cha pamoja (Block Farming), chenye jumla ya ekari 22,000 katika kijiji cha Masigati wilayani humo.

Akitoa taarifa kwa Bodi ya Wakurugenzi wa TARI iliyotembelea shamba hilo, Kijiji cha Masigati wilayani Manyoni, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo, alisema mpango huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuongeza uzalishaji na tija wa mazao ya kimkakati ikiwamo korosho.

Alisema kuwa TARI imeanza kutekeleza maono serikali ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa vitendo kutoka tani 300,000 za sasa hadi milioni moja ifikapo 2024 na ili kufanikisha wanatekeleza kwa kutumia mbinu bora za kilimo, matumizi ya mbegu bora na viutilifu katika mikoa hiyo mipya ikiwamo wa Singida.

“Tunataka kumtoa mkulima kutoka hali ya chini kabisa ili awe bilionea kupitia mazao ya kimkakati kupitia kilimo na korosho ndio itawatoa wakulima wa mkoa wa Singida kwa kuwa inaonyesha inastawi vizuri ikilinganishwa na mazao mengine, ndio maana TARI imeamua kuweka nguvu ya kutosha katika mkoa huu,” alisema.

Alisema TARI inataka kumtoa mkulima kutoka kilimo cha kujikimu na kufanya cha kibiashara ili aweze kuwekeza na kunufaika kupitia kilimo hicho na kuchangia uchumi wa mkulima mmoja mmoja pamoja na uchumi wa taifa kupitia zao hilo la korosho.

Mwenyekiti wa Bodi ya TARI, Dk. Yohana Budeba, alisema Bodi hiyo imejipanga kuhakikisha maagizo ya Rais Dk. John Magufuli, yanatekelezwa kwa wakati ikiwamo ya kupanua zao la korosho kutoka mikoa mitano iliyokuwa ikilimwa na kufikia 20 na utekelezaji umeshaanza kwenye mikoa hiyo mipya.

Alisema mwanzoni korosho ilikuwa ikilimwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Tanga na Pwani, lakini kupitia Bodi ya TARI sasa hivi wameshafika mikoa 20 ya hapa nchini lengo lake ni kuongeza malighafi zinazohitajika katika Viwanda hapa nchini asilimia 60 itoke kwenye kilimo.

“Bodi ya TARI itahakikisha inasimamia ili mipango yote ya serikali pamoja na maagizo yake yote yanafikiwa ikiwamo ya kuzalisha ajira kwenye viwanda kwa kupitia malighafi za kilimo ili kuinua uchumi wa nchi,” alisema Mwenyekiti huyo wa bodi.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa, alisema waliamua kuja na mkakati wa kilimo cha korosho kama zao mbadala la biashara kama mengine ya ufuta na dengu ili kuinuka kiuchumi baada ya watafiti kutoka TARI kuwahakikishia zao hilo kustawi kwa wingi katika mkoa huo.

Alisema kwa kuanzia walimua kufungua shamba lenye ukubwa wa ekari 22,000 kwaajili ya kufanya kilimo cha pamoja na kuagiza mbegu bora za korosho kutoka TARI Naliendele pamoja na kupatiwa wataalamu wa kutoa elimu ya zao hilo.

Naye Mkurugenzi wa TARI Naliendele, mkoani Mtwara, Dk. Fortunatus Kapinga, alisema Mkoa wa Singida ni miongoni mwa itakayofanya vizuri kwenye uzalishaji wa korosho na Tanzania kuliteka soko la dunia.

Habari Kubwa